May 30, 2016 15:42 UTC
  • Rais wa zamani wa Chad ahukumiwa kifungo cha maisha jela Senegal

Mahakama maalumu nchini Senegal imemhukumu kifungo cha maisha jela mtawala wa zamani wa kijeshi wa Chad, Hissene Habre baada ya kumpata na hatia ya kuhusika na kutenda jinai dhidi ya binadamu, utesaji na utumwa wa ngono.

Hukumu hiyo imetolewa leo baada ya waathirika na watetezi wa haki za binadamu kuendesha kampeni kwa muda wa miaka 16 za kupigania kiongozi huyo wa zamani wa Chad afikishwe kwenye vyombo vya sheria nchini Senegal alikokimbilia baada ya kuondolewa madarakani mwaka 1990 katika mapinduzi ya kijeshi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanamtuhumu Hebre mwenye umri wa miaka 72 kuhusika na mauaji ya watu 40,000 wakati wa utawala wake kuanzia mwaka 1982 hadi 1990.

Kesi ya Hissene Habre ilisikilizwa katika mji mkuu wa Senegal, Dakar na mahakama maalumu ya jinai iliyoundwa na Umoja wa Afrika kulingana na mfumo wa mahakama wa nchi hiyo.

Reed Brody, wakili wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambaye ametumia muda wa miaka 15 kuendesha kampeni kwa kushirikiana na waathirika ili kuhakikisha Habre anafikishwa mbele ya vyombo vya sheria amesema kesi hiyo ya kihistoria itawashajiisha watu wengine kuchukua hatua kama hizo katika kuwafatilia watu wengine walio sawa na Hissene Habre.../

Tags