Magaidi 2 wa al-Shabaab wauawa wakijaribu kushambulia uwanja wa ndege Somalia
Wanachama wawili wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab wameangamizwa walipojaribu kushambulia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aden Adde katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Maafisa usalama mjini Mogadishu wamesema magaidi hao waliuawa walipojaribu kuishambulia kambi ya jeshi katika uwanja huo wa ndege, kwa kutumia silaha ndogo ndogo na magurunedi.
Vyombo vya habari vya Somalia vimeripoti kuwa, askari polisi watatu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi lililotibuliwa.
Hata hivyo kundi hilo la kitakfiri bila kutoa ushahidi wowote limedai kuwa, limeua na kujeruhi askari wengi wa serikali katika tukio hilo la jana Jumatano, na eti shambulio lao limetimiza malengo yake.
Msemaji wa al-Shabaab, Abdiasis Abu Musab amedai kuwa wanachama wa genge hilo la kigaidi walifanikiwa kupenye katika kambi ya jeshi na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aden Adde katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuua idadi kubwa ya watu wakiwemo maafisa usalama.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya jeshi la Somalia kutangaza kuwa limewauwa wanamgambo saba wa kundi hilo la kigaidi mjini Kismayo kusini mwa nchi. Kwa muda sasa aghalabu ya maeneo ya Somalia hususan ya kusini mwa nchi hiyo yamekumbwa na ukosefu wa amani.