Mar 24, 2022 03:31 UTC
  • Wanachama 7,000 wa Boko Haram, ISWAP wajisalimisha Nigeria

Wanachama wasiopungua 7,000 wa kundi la kigaidi la Boko Haram na wenzao wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh tawi la Afrika Magharibi (ISWAP) wamejisalimisha kwa maafisa usalama katika kipindi cha wiki moja iliyopita kaskazini mwa Nigeria.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Christopher Musa, kamanda anayeongoza operesheni za kijeshi dhidi ya magenge ya kigaidi katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi.

Ameeleza kuwa, kuendelea kujisalimisha wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram na ISWAP ni ishara ya wazi ya mafanikio ya jeshi katika vita vyake dhidi ya magaidi hao.

Amesema waliojisalimisha watafanyiwa uchunguzi wa kina na vyombo vya usalama, na kisha kupelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia kabla ya kuruhusiwa kurudi tena katika jamii.

Wanachama wa ISWAP; maelfu miongoni mwao wamejilisamisha kwa serikali

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh. 

Mgogoro wa Boko Haram umeshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad. Genge la kigaidi la Boko Haram lilipanua mashambulizi yake pia hadi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger mwaka 2015 na hivyo kuhatarisha maisha ya watu katika maeneo hayo.

Tags