Waasi 27 wa ADF wauawa katika operesheni ya askari wa DRC
Askari wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) wamefanikiwa kuwaangamiza makumi ya wanamgamo wa kundi la ADF kaskazini mashariki mwa nchi.
Msemaji wa Jeshi la DRC katika mkoa wa Ituri, Luteni Jules Ngongo amesema waasi zaidi ya 27 wameuwa katika operesheni ya askari wa serikali katika kijiji cha Walese-vonkutu, kilichoko katika mkoa huo wa kaskazini mashariki.
Amesema jeshi la DRC limefanikiwa kukomboa ngome tatu za wapiganaji hao, mbali na kutegua mabomu na kutwaa silaha zingine zilizokuwa mikononi mwa waasi hao.
Msemaji wa Jeshi la DRC mkoani Ituri ameongeza kuwa, operesheni hiyo iliyoanza Jumatano iliyopita itaendelea hadi wahakikishe kuwa maeneo yote ya mkoa huo yanapata utulivu na uthabiti.
Katikati ya mwezi huu wa Machi, watu wasiopungua 27 waliuawa katika eneo la Beni huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika shambulio jipya la wanamgambo hao wanaotokea Uganda.
Aidha mwishoni mwa Januari mwaka huu, raia wengine 12 waliuawa katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi hao wa ADF.
Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.