Kongo DR: Waasi wa M23 wameitungua helikopta ya MONUSCO
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) limetangaza kuwa, helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa na askari jeshi wa kulinda amani wanane ilitunguliwa jana ikiwa katika shughuli ya kutathmini harakati za raia huko Kivu Kusini.
Ni baada ya Jeshi la Pakistan kutangaza jana usiku kuwa wanajeshi wake kadhaa wamefariki dunia katika ajali ya helikopta ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taarifa ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeeleza kuwa, helikopta hiyo iliyotunguliwa ilikuwa moja ya helikopta mbili za upelelezi za kikosi cha MONUSCO na ilikuwa imewabeba askari jeshi wanane wa kofia bluu pamoja na waangalizi wa Umoja wa Mataifa.
Helikopta ya MONUSCO imetunguliwa huku mapigano kati ya kundi la waasi wa M23 na Jeshi la Kongo yakiendea baada ya mashambulizi kadhaa Jumapili iliyopita katika maeneo ya Tchanzu na Runyonyi huko Rutshuru katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Wanajeshi kadhaa wa Kongo walijeruhiwa katika mapigano hayo makali yaliyowalazimisha makumi ya wenyeji wa maeneo hayo kukimbia nyumba zao.
Khassin Diage, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Masuala ya Ulinzi na Oparesheni ameeleza kuwa, amezungumza na Gavana wa Kivu Kaskazini na kwamba wamewapokea askari majeruhi huko Bunagana katika kambi ya kijeshi kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.
Habari zinasema kuwa, mapigano mapya kati ya kundi la waasi la M23 na Jeshi la Kongo yamelazimisha idadi kubwa ya raia kuhama makazi yao.
Jana Jumanne Jeshi la Kongo lililituhumu jeshi la Rwanda kuwa linawaunga mkono waasi walioibuka upya katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko Mashariki mwa Kongo; tuhuma ambazo zimekanushwa na Kigali.