Mamia ya Waethiopia warudishwa kwao kutoka Saudia baada ya mateso makubwa
Mamia ya raia wa Ethiopia jana Jumatano waliwasili Addis Ababa mji mkuu wa nchi hiyo, hilo likiwa kundi la kwanza la raia wapatao 100,000 kurejeshwa nyumbani wakitokea Saudi Arabia.
Takriban watu 900 waliorejea nchini Ethiopia, wakiwemo wakina mama wengi wenye watoto wadogo, jana walitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa wakitokea nchini Saudia. Hayo yameelezwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM). Shirika hilo limesema, linakadiria kuwa Waethiopia wasiopungua 750,000 kwa sasa wanaishi nchini Saudi Arabia na kwamba kuna uwezekano yapata 450,000 waliingia nchini humo kupitia njia zisizo za kawaida; hiyo watahitaji msaada ili kurejea nyumbani.
Mashirika ya haki za binadamu kwa miaka kadhaa sasa yamekuwa yakikosoa na kupinga mazingira na hali mbaya inayowakabili raia wa Ethiopia waliohajiri nchini Saudi Arabia. Jemila Shafi raia wa Ethiopia mwenye umri wa miaka 29 ambaye ni mmoja wa watu waliorejea nyumbani kutoka Saudia amesema walikuwa wakilia kila siku kutokana na hali mbaya na kwamba serikali ya Saudia ilikuwa ikiwapatia mkate moja na sufuria moja la wali kwa ajili ya 300. Anasema watu 400 walikuwa wakiishi kwenye chumba kimoja katika hali ya msongamano na kushindwa hata kuona mwanga wa jua.
Hana Yeshingus mwakilishi wa Wizara ya Wanawake na Watoto ya Ethiopia ameeleza kuwa ni raia hao wamerudi nyumbani baada ya kupitia machungu makubwa nchini Saudi Arabia.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita Saudi Arabia imewarejesha nyumbani karibu raia 352,000 wa Ethiopia.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesisitiza kuwa "kukidhi mahitaji ya watu 100,000 wanaorejea nyumbani itakuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Ethiopia, IOM, na washirika wao."