Wanajeshi 8 wa Mali wauawa katika shambulio la wabeba silaha
Askari wasiopungua wanane wa jeshi la Mali wameuawa baada ya kuviziwa na kushambuliwa na genge moja la wabeba silaha katika mji wa Bandiagara, eneo la Mopti, katikati mwa nchi hiyo.
Jeshi la Mali limethibitisha habari ya kuuawa askari wake wanane na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio hilo la Jumatano.
Limesema wanajeshi hao walivamiwa na genge la wabeba silaha wasiojulikana walipokuwa wakilinda doria baina ya wilaya ya Songoiba na Yaokanda katika eneo la Bandiagara, yapata kilomita 600 kusini mwa Bamako, mji mkuu wa nchi hiyo.
Mapema mwezi Machi, magenge yenye silaha yalishambulia kambi ya kijeshi katikati ya Mali na kuua wanajeshi 27 wa serikali, huku magaidi 47 wakiangamizwa kwenye shambulio hilo.
Mashambulizi ya makundi mbalimbali yenye misimamo mikali hususan wanachama wa mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la Daesh (ISIS) yameshtadi katika miezi ya karibuni katika maeneo mbalimbali huko Mali.
Nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika imekuwa ikipambana na magenge ya kigaidi huku karibu thuluthi mbili ya ardhi ya nchi hiyo ikiwa nje ya udhibiti wa serikali.