Wahajiri wengine 90 wafa maji katika ajali Bahari ya Mediterania
(last modified Mon, 04 Apr 2022 10:58:54 GMT )
Apr 04, 2022 10:58 UTC
  • Wahajiri wengine 90 wafa maji katika ajali Bahari ya Mediterania

Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amezitaka nchi za Ulaya kuwa na ukarimu na kuamiliana vyema na wakimbizi wengine, kama zinavyoamiliana na wakimbizi wa Ukraine.

Filippo Grandi amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter, baada ya wahajiri wengine zaidi ya 90 kuaga dunia kwenye ajali ya boti katika Bahari ya Mediterania.

Grandi ameandika: Watu zaidi ya 90 wameaga dunia kwenye mkasa mwingine (Bahari ya) Mediterania. Ulaya imethibitisha uwezo wa kuwapokea kwa ukarimu na moyo mkunjufu wakimbizi milioni 4 kutoka Ukraine. Sasa inapaswa kutathmini namna ya kuwapokea wahajiri na wakimbizi wengine wanaobisha mlangoni kwao.

Ulaya inavyowapokea kwa wingi na moyo mkunjufu wahajiri wa Ukraine

Mwito wa Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa unakuja baada ya Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) kutangaza habari ya kuaga dunia wahajiri zaidi ya 90 katika maji ya kimataifa, baada ya kuondoka Libya wakiwa kwenye boti iliyokuwa imejaa kupindukia siku kadhaa nyuma.

MSF imezitaka nchi za Ulaya za Malta na Italia kuwapokea manusura wa ajali hiyo na wahajiri wengineo wanaotokea Libya. Libya imekuwa ikitumiwa kwa muda sasa na makumi ya maelfu ya wahajiri kama moja ya malango makuu ya kuvukia na kuelekea Ulaya.