Watoto 6 miongoni mwa wahajiri 13 waliokufa maji Tunisia
Watoto 6 miongoni mwa wahajiri 13 waliokufa maji baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Tunisia, wakijaribu kuelekea Italia.
Mourad Turki, msemaji wa Idara ya Mahakama katika mji wa Pwani wa Sfax, yapata kilomita 270 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Tunisia, Tunis amesema wahajiri hao kutoka nchi za chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika waliaga dunia baada ya boti mbili walizokuwa wakisafiria kuzama katika Bahari ya Mediterania.
Turki ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, shughuli ya kutafuta miili ya wahajiri wengine wanaoaminika kuzama katika ajali hiyo ingali inaendelea, na kwamba mpaka kufika jana, miili 37 ilikuwa imeopolewa majini.
Gadi ya Pwani ya Tunisia hutekeleza operesheni karibu kila siku kuwazuia wahajiri wanaotumia nchi hiyo kuvuka Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya kinyume cha sheria.
Takwimu za Shirila la Kimataifa la Wahajiri (IOM) zinaonesha kuwa, wahajiri karibu 3,000 walikufa maji baharini wakati wakijaribu kuelekea barani Ulaya kwa kutumia maeneo ya kaskazini mwa Afrika mwaka jana 2021, na hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia 155 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Idadi kubwa ya wahajiri hao walipoteza maisha katika Bahari ya Mediterania mwaka jana walikuwa raia kutoka nchi za Tunisia, Algeria, Libya na Morocco.