Waasi wa M23 watangaza kuondoka katika vijiji vya Mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82380-waasi_wa_m23_watangaza_kuondoka_katika_vijiji_vya_mashariki_mwa_kongo
Waasi wa harakati ya M23 wametengaza kuondoka katika vijiji walivyoviteka wiki iliyopita huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mapigano kati yao na vikosi vya serikali mkoani Rutshuru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2022 03:05 UTC
  • Waasi wa M23 watangaza kuondoka katika vijiji vya Mashariki mwa Kongo

Waasi wa harakati ya M23 wametengaza kuondoka katika vijiji walivyoviteka wiki iliyopita huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mapigano kati yao na vikosi vya serikali mkoani Rutshuru.

Mapigano kati ya waasi hao na wanajeshi wa serikali ya Kinshasa yaliibuka Jumatano iliyopita baada ya kusita kwa siku kadhaa; ambapo waasi hao wa M23 walifanikiwa kuvidhibiti vijiji visivyopungua 12 katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini. 

Vijiji vilivyorejeshwa na waasi huko Kivu Kaskazini 

Kundi hilo limesema, wapiganaji wake wameamua kuondoka katika vijiji hivyo ili kuruhusu juhudi za kupatiwa ufumbuzi masuala yaliyopo kati yao na serikali kupitia mazungumzo ya wazi na yatakayozaa matunda. Waasi wa harakati ya M23 wamesema kuwa hawajawahi kuwa na nia ya kuteka na kuyadhibiti maeneo yoyote bali lengo lao pekee ni kutatua kwa amani mgogoro uliopo. 

Hata hivyo upande wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bado haujathibitisha kama kweli waasi hao wameondoka katika vijiji hivyo au la. 

Taarifa ya M23 imeongeza kuwa, harakati hiyo ina mpango wa kuwakabidhi kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu wanajeshi wote wa jeshi la Kongo iliowateka nyara vitani ili wapate huduma zinazotakiwa. 

Harakati hiyo ya waasi iliasisiwa na wanachama wa zamani wa kundi la wanamgambo wa Kitutsi wa Kongo ambao kwa wakati fulani walikuwa wakiungwa mkono na nchi za Uganda na Rwanda.