Wanigeria waandamana kutaka Zakzaky apewe paspoti yake
Wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, kuishinikiza serikali ya nchi hiyo impe Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo pasipoti yake ya kusafiria iliyotwaa.
Waandamanaji hao walikusanyika nje ya ofisi za Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Nigeria, ambapo walisikika wakipiga nara za kulaani hatua ya serikali ya kuendelea kuzuia pasi ya kusafiri ya Sheikh Zakzaky na mkewe Malama Zenat.
Wamesema kiongozi huyo wa kidini aliwekwa kizuizini katika mazingira magumu kwa zaidi ya miaka mitano licha ya hali yake mbaya ya kiafya, lakini hatimaye mahakama ikamuachia huru.
Waandamanaji hao wamesema ikilazimu, watarejea tena mabarabarani kufanya maandamano ya mara kwa mara kushinikiza kuachiwa paspoti ya Sheikh Zakzaky ambaye anataka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Wamesema kuna dharura mwanachuoni huyo wa Kiislamu na mkewe kupewa pasi zao za kusafiria ili wakatafute matibabu nje ya nchi, kutokana na hali mbaya ya afya inayowakabili.
Sheikh Ibrahim Zakzaky alijeruhiwa vibaya sana wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanachuoni huyo katika mji wa Zaria mnamo Disemba 2015.