Kenya yahimiza kufungwa kambi kubwa ya wakimbizi duniani ya Dadaab
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya amesema kuwa, kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo itakuwa imefungwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Joseph Nkaissery amesema hayo wakati alipozungumza na vyombo vya habari kuwa Kenya imejiandaa kutekeleza makubaliano ya pande tatu yaliyosainiwa na pande kadhaa ili kuwarejesha makwao wakimbizi salama usalimini na katika mazingira ya kibinadamu. Waziri Nkaissery amesema, anapenda kuutangazia ulimwengu kuwa uamuzi wa kuifunga kambi ya Dadaab umefikia mwisho.
Kenya imetoa dola milioni kumi kufadhili zoezi hilo, ambalo Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo amesema kuwa ni lazima litekelezwe kufuatia vitisho vya usalama vilivyopo kutokana na kuwepo kambi hiyo. Kambi kuu ya wakimbizi duniani ya Dadaab iliasisiwa mwaka 1991 kwa madhumuni ya kutoa hifadhi kwa familia zinazokimbia vita na machafuko huko Somalia. Baadhi ya familia hizo zimeishi katika kambi hiyo kwa zaidi ya miaka 20.