Burundi: Uhusiano na Rwanda utaimarika zaidi ikitukabidhi wahusika wa jaribio la mapinduzi
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi, amesema uhusiano wa nchi yake na Rwanda utakuwa mzuri zaidi iwapo watu waliopanga na kufadhili jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya 2015 wanaodhaniwa kuwa wako mafichoni jijini Kigali watarejeshwa mjini Gitega kufunguliwa mashtaka.
Akizungumza katika Ikulu yake jijini Bujumbura,rais Ndayishimiye ameeleza kuwa Burundi inafanya mazungumzo na mamlaka nchini Rwanda ili kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki ambao umeyumba kwa kipinidi cha miaka 7 iliyopita.
Mataifa hayo jirani hayajakuwa na uhusiano mzuri kwa miaka kadhaa sasa, Burundi ikifunga mipaka yake; na Rwanda ikipiga marafuku uuzaji wa matunda na mbogamboga za Burundi jijini Kigali tangu mwaka 2016.
Tangu kuingia madarakani kwa rais Ndayishimiye 2020, uhusiano kati ya Kigali na Bujumbura umeonekana kuanza kuimarika kwa kiasi kikubwa.

Ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu wa mataifa hayo mawili wakiwemo wakuu wa intelijensia na magavana wamekuwa wakikutana kwa lengo la kujenga urafiki tena.
Waziri Mkuu wa Rwanda Edouard Ngirente, alifanya zaira jijini Bujumbura wakati wa sherehe za Siku ya Uhuru wa Burundi Julai 2021. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu wa Rwanda kuzuru Burundi tangu mzozo kwa kisiasa kuanza kati yao mwaka 2015.
Mwaka 2021, Burundi katika taarifa yake ilisema kuwa hatua kubwa zilikuwa zimepigwa kuelekea uimarishwaji wa amani na usalama kati ya Rwanda na Burundi.
Burundi ilitoa mchango mkubwa kwa Rwanda wakati ilipowakamata na kuwakabidhi kwa Kigali magaidi waliokuwa wanapanga shambulio nchini Rwanda.
Rwanda na yenyewe Julai 2021 iliwakabidhi Burundi watu 19 wenye silaha waliokuwa wametekeleza shambulio nchini Burundi na baadae kutorekea nchini Rwanda.../