Shambulizi jipya la kigaidi laua watu 8 nchini Mali
Kwa akali watu wanane wameuawa katika shambulzi jipya la kigaidi lililotokea kusini mwa Mali.
Duru za habari zimeripoti kuwa, genge lisolojulikana la wabeba silaha jana Jumapili lilishambulia watu katika kituo hicho cha usalama kilichoko katika jiji la Koutiala kusini mwa Mali, na kuua watu wanane, na kujeruhi wengine wanane.
Habari zaidi zinasema kuwa, mtu mmoja hajulikana aliko baada ya magaidi hao kushambulia kituo hicho cha upekuzi kusini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya askariwawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, kuuawa katika mji wa Douentza ulioko mkoa wa Mopti kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Bamako.
Magaidi wa makundi ya ukufurishaji yanayofungamana na ISIS au Al Qaeda wamekuwa wakitekeleza mashambulizi dhidi ya raia na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu sasa katika eneo la Ziwa Chad, magharibi mwa Afrika.
Mgogoro wa hali mbaya ya kiusalama umeigubika Mali tangu mwaka 2012; na vikosi vya majeshi kutoka nje hasa vya Ufaransa vilivyotimuliwa hivi karibuni havijaweza kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo.