Wafanyakazi wa afya na walimu waanzisha mgomo Zimbabwe kulalamikia hali zao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i84992-wafanyakazi_wa_afya_na_walimu_waanzisha_mgomo_zimbabwe_kulalamikia_hali_zao
Wafanyakazi wa sekta za afya na ualimu nchini Zimbabwe wameanzisha mgomo kulalamikia mazingira duni ya kazi huku wakikataa nyongeza ya asilimia mia moja ya mishahara iliyotangazwa na serikali mwishoni mwa wiki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 21, 2022 13:46 UTC
  • Wafanyakazi wa afya na walimu waanzisha mgomo Zimbabwe kulalamikia hali zao

Wafanyakazi wa sekta za afya na ualimu nchini Zimbabwe wameanzisha mgomo kulalamikia mazingira duni ya kazi huku wakikataa nyongeza ya asilimia mia moja ya mishahara iliyotangazwa na serikali mwishoni mwa wiki.

Wafanyakazi wa sekta ya afya, wakiwemo wauguzi, madaktari wadogo na wataalamu wa kitengo cha picha wamekusanyika kwenye hospitali kubwa zaidi ya umma ya Parirenyatwa Group of Hospitals katika mji mkuu Harare kwa ajili ya kuanza mgomo wao usio na kikomo.

Jumuiya zinazowakilisha wafanyakazi wa sekta ya afya wamesema, mgomo huo ulioanza jana ndio hatua ya mwisho ambayo zimelazimika kuchukua baada ya serikali kukataa kuzungumza nao tangu mwezi Aprili mwaka jana.

Akihutubia hadhara ya wafanyamgomo, kiongozi wa Baraza la Afya Tapiwanashe Kusotera amesema waziri wa Afya na Matunzo ya Mtoto, ambaye pia ni makamu wa rais Constantino Chiwenda hajakutana na mwajiriwa yeyote wa sekta ya afya huku serikali ikiendelea kueleza uongo unaokinzana na uhalisia wa mambo.

"Wamekataa kutusikiliza na sisi tumekataa kufanya kazi", amesisitiza Kusotera.

Thamani ya sarafu ya Zimbabwe imeshuka sana

Mgomo huo ni wa pili kufanywa na wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Zimbabwe tangu mripuko wa ugonjwa wa Covid-19 ulipoanza nchini humo 2020.

Watumishi wa umma wamekuwa wakishinikiza mishahara yao iangaliwe upya kutokana na ughali mkubwa wa bidhaa ulioikumba Zimbabwe ambao ulifikia asilimia 131.7 katika mwezi uliopita wa Mei.

Wafanyakazi hao serikali wanataka mishahara yao ilipwe kulingana na sarafu ya dola ya Marekani kutokana na dola ya Zimbabwe kuyumba mno.

Sambamba na sekta ya afya, jumuiya nne zinazowakilisha walimu nchini Zimbabwe nazo pia zimetangaza kuwa wafanyakazi wao hawatafika makazini kwa muda wa siku tano kulalamikia mazingira duni ya kazi. Mgomo huo ulianza jana Jumatatu na utaendelea hadi Jumamosi ya tarehe 25 Juni.../