Wakongo wanasubiri kupokea jino la shujaa wa uhuru, Patrice Lumumba
Wakazi wa mji alikozaliwa shujaa wa uhuru wa Kongo, Patrice Lumumba, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanasubiri kurejeshwa jino la kinara huyo wa uhuru wa nchi yao ambalo ndio mabaki pekee ya mwili wake yaliyosalia baada ya kuuliwa na wakoloni wa Kibelgiji wakishirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA.
Wakazi wa mji huo alikozaliwa Lumumba wanasubiri kupokea jino hilo ikiwa imepita miaka 62 baada ya kifo chake. Jino hilo la dhahabu awali lilikabidhiwa kwa familia ya Lumumba nchini Ubelgiji, huku mkoloni huyo wa zamani wa Kongo akifanya jitihada za kutafuta mariadhiano na Wakongo. Maurice Tasombo Omatuku ndugu wa familia ya Patrice Lumumba amenukuliwa akisema kuwa: "Lumumba alijitolea maisha yake kwa ajili ya Wakongo na kwamba wanaitaka serikali ya Ubelgiji ijenge mnara wa kumbukumbu ya kihistoria ambapo vizazi vijavyo vitaweza kushuhudia.
Jeneza lenye jino hilo linazamiwa kusafirishwa hadi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo baadaye litazikwa rasmi katika eneo maalumu la kumbukumbu.
Wakati huo huo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa, inajiandaa kuwa na siku tatu za maombolezo kuanzia tarehe 27 hadi 30 mwezi huu wa Juni, katika maadhimisho ya kutimia mwaka wa 62 wa uhuru wa nchi hiyo sambamba na kufanyika shughuli ya mazishi.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, jino hilo la dhahabu ni mabaki pekee ya mwili wa Lumumba ambaye aliuawa na wakoloni hao wa Ubelgiji waioshirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA, na kisha mwili wake ukayeyushwa kwa tindikali hapo mwaka 1961.
Ubelgiji ilikiri kuhusika na mauaji ya ya Lumumba miaka 40 baada ya tukio hilo; na shirika la ujasusi la Marekani CIA ndilo lililopanga njama ya kumuua mwanasiasa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 35.
Wakoloni wa Kibelgiji walifanya ukatili mkubwa na wa kutisha nchini Congo na inakadiriwa kuwa raia wasiopungua milioni kumi wa nchi hiyo waliuawa katika kipindi cha utawala wa wakoloni hao.
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo amesisitiza kwamba mamlaka ya nchi yake inawajibika kimaadili kuhusiana na mauaji hayo.