Sisitizo la kuendeshwa mapambano ya pande zote dhidi ya ugaidi barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8512-sisitizo_la_kuendeshwa_mapambano_ya_pande_zote_dhidi_ya_ugaidi_barani_afrika
Rais wa Senegal amezitolea mwito serikali mbalimbali kushirikiana na kukusanya nguvu na nyezo zote ili kupambana na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2016 06:28 UTC
  • Sisitizo la kuendeshwa mapambano ya pande zote dhidi ya ugaidi barani Afrika

Rais wa Senegal amezitolea mwito serikali mbalimbali kushirikiana na kukusanya nguvu na nyezo zote ili kupambana na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada.

Rais Macky Sall wa Senegal alisema jana mjini Dakar katika kikao cha wakuu wa nchi za Magharibi mwa Afrika kuwa, mashambulizi yanayojiri kaskazini mwa Mali, Niger na Nigeria yanaonyesha kuwa, ni dhahir shahir kuwa vitisho vya ugaidi ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa huko magharibi mwa Afrika. Rais wa Senegal ambaye alikuwa mwenyeji wa kikao cha 49 cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika amesema kuwa kunapaswa kuwepo ushirikiano wa pamoja na kuandaliwa suhula zote ili kudhamini usalama barani Afrika.

Rais Sall ameyatamka hayo baaada ya makumi ya wanajeshi kuuliwa na kujeruhiwa katika shambulio la umwagaji damu siku mbili zilizopita katika kitongoji ch Bosso kusini mashariki mwa Niger.

Wakazi wa nchi nyingine za Magharibi mwa Afrika pia wamekuwa wakiishi katika hali ngumu kutokana na kukabiliwa na hali ya mchafukoge na vitendo vya kigaidi.

Pamoja na kufanyika vikao mbalimbali vya kutokomeza ugaidi katika eneo na pia kutekelezwa juhudi za kuboresha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Magharibi mwa Afrika, lakini inaonekana kuwa hadi kufikia sasa nchi hizo hazijapata mafanikio ya kuridhisha.

Vitendo vya kigaidi vya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada huko kaskazini mwa Mali, Niger na katika nchi nyingine za eneo vingali vinaendelea; na katika upande wa pili hali ya ukosefu wa amani katika eneo imesababisha sehemu kubwa ya bajeti ya nchi za ukanda huo kutumika katika manunuzi ya silaha na zana za kijeshi kwa minajili ya kupambana na ugaidi. Kwa msingi huo katika sekta za kiuchumi pia, hakuna uwekezaji wa kutosha uliofanywa na serikali za eneo na umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na kudorora uchumi ni matatizo ambayo yanawasumbua sana wakazi wa eneo hilo.

Hii ni katika hali ambayo jukumu kuu linalozikabili nchi za Magharibi mwa Afrika ni kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi na makundi yenye misimamo mikali; huku weledi wa mambo wakiamini kuwa, kutekelezwa marekebisho, kuboreshwa sekta ya uchumi khususan kubuniwa nafasi za ajira kwa vijana, kuwepo ustawi wa kitamaduni na kijamii, ni masuala yanayoweza kuinua jamii na kuzuia kujiri vitendo vya ugaidi.

Iwapo nchi za eneo hilo zitafungamana na shaari za kuzidisha na kuimarisha ushirikiano wa kieneo katika nyanja mbalimbali khususan katika uwanja wa kiuchumi; basi ushirikiano huu utaweza kubadili hali ya sasa ya kiuchumi na kisiasa katika nchi hizo na kuzifanya kupiga hatua katika kalibu ya ushirikiano wa pamoja wa kieneo.

Hakuna shaka kuwa harakati za makundi ya kigaidi na yale yenye misimamo ya kuchupa mipaka zitakabiliwa na hali ngumu na kusambaratika katika mazingira kama hayo, iwapo kutaasisiwa mfumo sahihi wa kiuchumi na kisiasa katika eneo. Hata hivyo baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa kuitishwa vikao kama hivyo na viongozi wa nchi za Kiafrika, kivitendo hakutakuwa na maslahi kwa watu wa eneo hilo. Hii ni kwa sababu hatua zinazotekelezwa na baadhi ya viongozi wa nchi hizo ni miamala yenye lengo la kuwadhaminia maslahi binafsi na kulinda madaraka yao na hivyo kufanyika vikao hivyo kwa hakika ni mchezo wa kimaonyesho tu. Hivi sasa inaonekana kuwa viongozi wa nchi za Magharibi mwa Afrika wana fursa ndogo ya kubadili mitazamo na kufanya juhudi za dhati za kuboresha hali ya mambo na kuleta ustawi katika nchi hizo katika nyanja mbalimbali.