Wizara ya Mambo ya Ndani Tunisia: Kuna njama ya kumuua Kais Saied
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i85130-wizara_ya_mambo_ya_ndani_tunisia_kuna_njama_ya_kumuua_kais_saied
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa ina taarifa za kuaminika zinazothibitisha kuwepo kwa vitisho vinavyolenga uhai wa Rais wa Jamhuri, Kais Saied.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jun 25, 2022 03:02 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Ndani Tunisia: Kuna njama ya kumuua Kais Saied

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa ina taarifa za kuaminika zinazothibitisha kuwepo kwa vitisho vinavyolenga uhai wa Rais wa Jamhuri, Kais Saied.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Tunis imevitaja vitisho hivyo kuwa ni vikubwa na kuzishutumu pande za ndani na nje kuwa ndizo zilizopanga njama za kumlenga rais wa Tunisia na Ofisi ya Rais.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imedokeza kuwa, imewakamata watu 3 wa chama cha "Namaa", na imekituhumu chama hicho kuwa kimepokea ufadhili kutoka nje ya nchi. Imeeleza kuwa watu kadhaa wamehusika katika tuhuma za ufadhili unaoshukiwa, na kusisitiza kuwa mafaili yao bado yanachunguzwa.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia pia imesema kwamba imezima kile ilichokitaja kuwa operesheni ya kigaidi, ambayo imesema, ililenga taasisi nyeti katikati mwa mji mkuu, na kumtia mbaroni mhusika.

Kwa upande wake, mkuu wa Jumuiya ya Uokoaji ya Tunisia, Najib Chebbi, ameviambia vyombo vya habari kwamba mkutano huo wa Wizara ya Mambo ya Ndani haukutoa taarifa zaidi kuhusu jaribio linalodaiwa kumlenga rais wa nchi hiyo na kuongeza kuwa "inasikitisha kuona kwamba masuala ya nchi ya Tunisia yanasimamiwa kwa njia hii."

Najib Chebbi

Chebbi amesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia inalenga kuandaa anga na mazingira ya kampeni kubwa ya kukamatwa kwa watu kiholela na itaathiri viongozi wa kisiasa na kiraia nchini Tunisia.

Tarehe 25 Julai 2021 Kais Saied alichukua madaraka ya Tunisia kwa njia inayoshabiana na mapinduzi kwenye nchi hiyo ndogo ya Afrika Kaskazini. Katika hatua ambayo haikutarajiwa wakati huo, Kais Saied alisimamisha Bunge na kumfuta kazi spika wake, pamoja na waziri mkuu wa serikali, na kuchukua udhibiti wa mambo yote ya nchi.