Maiti 20 za wahajiri zapatikana jangwani nchini Libya
Maiti 20 za wahajiri walioripotiwa kutoweka katika jangwa nchini Libya karibu na mpaka wa Chad, zimepatikana kusini mashariki mwa nchi.
Shirika la huduma za ambulensi la Kufra nchini Libya limesambaza mitandaoni picha inayoonesha miili ya wahajiri hao ikiwa imerundikana kwenye gari jeusi aina ya pick-up katika eneo lililoko baina ya jiji la Kufra na mpaka wa Chad.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, maiti hizo zimepatikana wiki mbili baada ya wahamiaji hao kupoteza mawasiliano wakiwa katika jangwa hilo la Libya.
Habari zaidi zinasema kuwa, yumkini wahajiri hao wameaga dunia kutokana na njaa na kiu, na kukata masafa marefu katika jangwa hilo lenye joto kali.
Visa vya kuaga dunia wahajiri wakiwa majangwani hususan jangwa la Sahara vimeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuweko wimbi kubwa la wahajiri wanaopita katika jangwa hilo wakielekea Libya na baadaye barani Ulaya.
Aghalabu ya wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, hutokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Niger Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia.