Marais wa EAC wajadili soko la pamoja Arusha, Somalia yataka uanachama
(last modified Fri, 22 Jul 2022 08:02:41 GMT )
Jul 22, 2022 08:02 UTC
  • Marais wa EAC wajadili soko la pamoja Arusha, Somalia yataka uanachama

Viongozi wa wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), wameashiria miaka 11 tangu kuanzishwa kwa itifaki ya soko la pamoja na kusisitiza kuwa, kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwepo kuongezeka kwa biashara, mitaji na ajira kwa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika na Mashariki.

Wakizungumza katika majadiliano juu ya mafanikio na changamoto ya soko la pamoja baina ya nchi wanachama, viongozi hao wamesema utangamano katika nchi za EAC umekuwa na manufaa makubwa na kutaka kuondolewa baadhi ya vikwazo vya kisera kwa baadhi ya nchi.

Mkutano huo wa wakuu wa jumuiya ya EAC ulianza jana Alkhamisi jijini Arusha nchini Tanzania, na unatazamiwa kumalizika leo Ijumaa.

Mwenyekiti wa EAC ambaye ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema moja ya mambo ambayo yamekuwa na manufaa ni uboreshwaji wa miundombinu katika nchi wanachama.

Rais Kenyatta amesema hivi sasa wananchi wa Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaunganishwa na barabara na miradi mingine ikiwemo ya umeme.

Naye Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumzia suala la uhakika wa chakula katika nchi za Afrika Mashariki amesema inawezekana kuongeza uzalishaji maradufu na kutosheleza mahitaji ya ndani na nje.

Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud

Amesema hata hivyo uwepo wa ardhi pekee hauwezi kuhakikisha uzalishaji unaongezeka bali pia uwepo wa mvua za kutosha, fedha lakini pia teknolojia. "Kuna haja ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kuwa na uwezo wa kuhifadhi vizuri mazao lakini pia kuwa na masoko ya uhakika ya mazao," amesema.

Wakati huohuo, Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud yupo jijini Arusha kuwasilisha ombi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika la kukubaliwa kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Siku chache zilizopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilipasishwa kuwa mwanachama kamili wa saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.

Tags