Misri mwenyeji wa luteka inayojumuisha US, Saudia, Ugiriki na Imarati
Vikosi maalumu vya majeshi ya Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ugiriki na Cyprus vimezindua mazoezi ya pamoja ya kijeshi nchini Misri.
Taarifa ya jeshi la Misri imesema, luteka hiyo ya kijeshi ilizinduliwa jana Jumapili, na kwamba Marekani, Jordan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Bahrain zinashiriki kama nchi watazamaji.
Luteka hiyo inafanyika katika kambi ya kijeshi ya Mohamed Naguib na vituo vingine vya mafunzo ya kijeshi katika Eneo la Kijeshi la Kaskazini, katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Taarifa ya jeshi la Misri imeongeza kuwa, maneva hiyo iliyopewa jina la Hercules-2022 itafanyika kwa siku kadhaa zijazo. Cairo inadai kuwa, mazoezi hayo ya kijeshi ni mwendelezo wa jitihada za kuimarisha uhusiano wa kijeshi wa Misri na nchi ndugu na rafiki.

Luteka hiyo inafanyika katika hali ambayo, uhusiano kati ya Uturuki na Ugiriki unazidi kuvurugika, huku pande mbili hizo zikizozana juu ya rasilimali ya gesi ya hydrocarbon na kutunishiana misuli mashariki mwa Mediterranean.
Uhusiano wa Uturuki na Misri pia ulikuwa umeingia doa kwa miaka kadhaa nyuma, lakini Aprili mwaka huu Ankara iliamua kumteua balozi wake wa Cairo, baada ya kupita miaka tisa ya mzozo wa kidiplomasia baina ya nchi mbili hizo.