Nchi za Afrika zapasisha stratejia ya kupambana na magonjwa sugu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87378-nchi_za_afrika_zapasisha_stratejia_ya_kupambana_na_magonjwa_sugu
Mawaziri wa Afya wa nchi za Afrika wameunga mkono stratejia mpya inayonuia kupiga jeki upatikanaji wa dawa na matibabu ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza barani humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 24, 2022 10:48 UTC
  • Nchi za Afrika zapasisha stratejia ya kupambana na magonjwa sugu

Mawaziri wa Afya wa nchi za Afrika wameunga mkono stratejia mpya inayonuia kupiga jeki upatikanaji wa dawa na matibabu ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza barani humo.

Mpango huo uliopewa jina la PEN-PLUS ulipasishwa jana Jumane na mawaziri hao katika mkutano wa Kamati ya Kieneo Afrika ya Shirika la Afya Duniani WHO uliofanyika Lome, mji mkuu wa Togo.

Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa kieneo wa WHO barani Afrika amesema, "Afrika inakabiliwa na mzigo mzito wa magonjwa sugu ambayo yanachukua uhai wenye thamani wa watu, licha ya kuwa yanaweza kutibika."

Dakta Moeti ameeleza bayana kuwa, kupasishwa kwa stratejia hiyo ni hatua moja mbele kwa ajili ya kuimarisha afya na siha ya mamilioni ya watu barani Afrika.

Taarifa ya Kamati ya Kieneo ya Afrika ya WHO imesema, magonjwa sugu yanaweza kusababisha viwango vya juu vya ulemavu na hata vifo hususan miongoni mwa watoto, vijana wanaobaleghe na hata mabarobaro.

Kwa mujibu wa utafiti wa WHO wa mwaka 2019, asilimia 36 tu ya nchi za Afrika ndizo zina dawa za kutegemewa za kutibu magonjwa sugu katika hospitali na zahanati za umma.

Mawaziri wa Afya wa Afrika wametoa mwito kwa serikali za nchi za bara hilo kuhakikisha kwamba dawa na matibabu ya magonjwa sugu yasiyoambukiza yanapatikana kwa wepesi katika hospitali na vituo vya afya vya umma.