Rais wa Tunisia akosoa uingiliaji wa mambo ya ndani wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87632-rais_wa_tunisia_akosoa_uingiliaji_wa_mambo_ya_ndani_wa_marekani
Rais wa Tunisia amekosoa vikali kile alichokitaja kuwa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya taifa hilo la Kiarabu la kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Aug 31, 2022 02:46 UTC
  • Rais wa Tunisia akosoa uingiliaji wa mambo ya ndani wa Marekani

Rais wa Tunisia amekosoa vikali kile alichokitaja kuwa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya taifa hilo la Kiarabu la kaskazini mwa Afrika.

Katika mazungumzo yake na Barbara Leaf, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika masuala ya kanda ya Mashariki, Rais Kais Saied amekosoa matamshi ya hivi karibuni ya maafisa wa Marekani kuhusu hali ya sasa ya Tunisia.

Rais huyo wa Tunisia amesisitiza kuwa: Tunapinga uingiliaji wa masuala yetu ya ndani. Tunisia inashikilia msimamo wake thabiti juu ya uhuru na mamlaka yake ya kujitawala.

Mwishoni mwa Julai pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ilimuita balozi mdogo wa Marekani mjini Tunis kulalamikia matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kuhusu kura ya maoni ya katiba iliyofanyika nchini humo hivi karibuni.

Maandamano ya kupinga kura ya maoni

Blinken alidai kuwa ana wasiwasi kuhusu demokrasia ya Tunisia baada ya Rais Kais Saeid kupendekeza katiba mpya inayompa mamlaka zaidi. Wakuu wa uchaguzi Tunisia wanasema asilimia 92.3 ya washiriki wa zoezi hilo la Julai 25, walipiga kura kuunga mkono rasimu ya katiba.

Rais wa Tunisia amewataka maafisa wa Marekani kuwasikiliza wenzao wa nchi hiyo ya Kiarabu ili kufahamu hali halisi ya mambo katika taifa hilo.