Kiongozi wa Mali ataka 'fidia' ili kuwaachia askari wa Ivory Coast
Rais wa mpito wa Mali amesema anataka suluhu yenye maslahi ya pande mbili ili kuhitimisha mkwaruzano wa kidiplomasia baina ya nchi hiyo na Ivory Coast.
Hayo yameripotiwa na televisheni ya serikali ya Mali na kufafanua kuwa, Rais wa Mpito Assimi Goita ameeleza bayana kuwa yuko tayari kuupatia ufumbuzi mzozo wa kidiplomasia baina ya nchi yake na Ivory Coast, uliotokana na kitendo cha Bamako kuwakamata makumi ya askari wa Kodivaa.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, "Goita angelipenda suluhisho lenye maslahi ya pamoja juu ya mzozo (wa askari wa Ivory Coast), na wala haungi mkono suluhu ya upande mmoja inayotaka Mali iachane na matakwa yake tena bila fidia."
Haya yanajiri siku chache baada ya Mali kuwaachia huru askari watatu wanawake kati ya askari 49 wa Ivory Coast waliokamatwa na kuwekwa kizuizini nchini humo miezi miwili iliyopita.
Askari hao wanawake waliachiwa huru zikiwa zimepita takribani wiki saba tangu wao na wenzao wanaume 46 walipokamatwa, hatua ambayo imezusha mzozo wa kidiplomasia kati ya Mali inayotawaliwa na jeshi na Ivory Coast.
Serikali ya kijeshi ya Mali ilisema, kundi la askari hao - ambao walizuiliwa katika uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Mali, Bamako mnamo Julai 10 - waliingia nchini humo bila kibali na walihesabiwa kuwa ni mamluki.
Ivory Coast, ambayo imekuwa ikiomba mara kwa mara askari wake waachiliwe huru, inasema wanajeshi hao hawakustahiki kukamatwa kwa sababu walitumwa kwenda kutoa msaada kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, MINUSMA. Serikali ya Yamoussoukro inasisitiza kuwa, mamlaka za Mali zina taarifa kamili kuhusu majukumu yaliyokuwa yatekelezwe na wanajeshi hao.