Marekani yapiga ngoma ya vita kwa kuipa Taiwan 'msaada' wa kijeshi
Bunge la Seneti la Marekani limepasisha muswada wa sheria inayotaka Taiwan kupewa msaada wa kijeshi wa mabilioni ya dola, hatua inayotazamiwa kuighadhabisha China.
Kamati ya Uhusiano wa Nje ya Seneti ya Marekani imepasisha muswada huo ambao, mbali na kutaka Taiwan kupewa na Washington msaada wa kijeshi wa dola bilioni 4.5 ndani ya miaka minne ijayo, unataka pia kuangalia upya Sera ya China Moja.
Kadhalika muswada huo unataka China kuwekewa vikwazo na Marekani, ili kuzuia eti mashambulizi tarajiwa ya kijeshi ya Beijing dhidi ya kisiwa cha Taiwan.
Ingawaje Seneta Bob Menendez ambaye anaongoza kamati hiyo ya Baraza la Seneti ya Marekani anadai kuwa muswada huo haumaanishi kuwa Marekani inataka vita au kushadidisha taharuki baina yake na China, lakini wadadisi wa mambo na viongozi wa Beijing wana mtazamo tofauti.
Iwapo muswada huo utapasishwa na Seneti, Baraza la Wawakilishi na kisha kuidhinishwa kuwa sheria na Rais Joe Biden, China itawekewa vikwazo vipya vinavyonuia kuzuia kabisa nchi za dunia kufanya biashara au kuwekeza na Beijing katika masuala hasasi ya kiteknolojia kama hifadhi ndogo za tarakilishi (microchip) na suhula za mawasiliano.

Hivi karibuni, China ilikosoa vikali mpango mpya wa serikali ya Marekani wa kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya dola bilioni 1.1, ikisisitiza kuwa mawasiliano yoyote ya kijeshi na Taipei ni ukiukaji wa kanuni ya "China Moja".
Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China, na imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taipei; na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.