AMISOM yaangamiza wanachama 110 wa al-Shabaab Somalia
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimesema askari wake wamefanikiwa kuangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab walipojaribu kushambulia moja ya kambi zao.
Luteni Kanali Joe Kibet, msemaji wa AMISOM ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, askari wa AMISOM wameangamiza wanamgambo 110 wa al-Shabaab na kunasa shehena ya silaha katika operesheni kali iliyojiri leo katika mji wa Halgan.
Kadhalika amekanusha madai yaliyotolewa na kundi hilo la kigaidi, kwamba wameua askari 60 wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM. Mapema leo wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabab walidai kuwa wameshambulia kambi ya jeshi ya askari wa Ethiopia nchini Somalia na kuua askari zaidi ya 43 wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Hata hivyo, Meja Abdifatah Elmi, kamanda mwandamizi wa jeshi la Somalia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kumejiri makabiliano makali kati ya al-Shabaab na jeshi la Somalia wakishirikiana na AMISOM katika mji wa Bulaburde na kwamba kuna maafa na majeruhi kutoka pande zote. Mashambulizi ya kigaidi yameshtadi nchini Somalia katika hali ambayo, nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inajiandaa kwa uchaguzi wa rais mwezi Agosti mwaka huu.