Walioaga dunia kwa mafuriko Nigeria wapindukia 500, Sudan Kusini 62
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na mafuriko huko nchini Nigeria imeongezeka na kufikia watu 500.
Msemaji wa Idara ya Kushughulikia Majanga nchini humo, Manzo Ezekiel ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mbali na watu zaidi ya 500 kufa maji, wengine zaidi ya milioni 1.4 wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko hayo.
Ameongeza kuwa, watu wasiopungua 1,546 wamejeruhiwa kutokana na thari za mafuriko hayo yanayotajwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo tangu 2012.
Afisa katika Wizara ya Masuala ya Binadamu nchini Nigeria, Nasir Sani-Gwarzo amesema serikali ya nchi hiyo inafanya kila liwezekanalo kuwafikishia misaada ya kibinadamu waathirika wa janga hilo la kimaumbile.
Idara ya Hali ya Hewa ya Nigeria imetahadharisha pia kuhusu mvua kali zitakazonyesha siku zijazo katika mikoa kadhaa ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Huku hayo yakijiri, watu 62 wamepoteza maisha kufikia sasa nchini Sudan Kusini kutokana na mafuriko makubwa yanayosababishwa na mvua kali zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Dakta Fabian Ndenzako, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Sudan Kusini amesema watu zaidi ya 630,000 wameathiriwa na mafuriko hayo katika kaunti 9 za nchi hiyo. Amesema maisha ya maelfu ya watu yako hatarini wakikodolewa macho na maradhi yanayosababishwa au kuenezwa kupitia maji machafu kama vile kipindupindu, surua na malaria.
Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema majimbo yaliyoathirika zaidi na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu Aprili mwaka huu ni Bahr el Ghazal Kaskazini, Warrap, Unity na Equatoria Magharibi.