Afrika mhanga wa matokeo na taathira ya migogoro ya kimataifa
Akthari ya mataifa ya Afrika ambayo katika miongo ya hivi karibuni yalifanya hima kubwa ya kujenga miundomsingi yao ya kiuchumi kwa minajili ya kuboresha hali ya uchumi wao, filihali yanahesabiwa kuwa wahanga wakubwa zaidi wa matukio ya sasa ulimwenguni.
Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umesema katika ripoti yake kwamba: Nchi za Kiafrika zilipaswa mwaka huu wa 2022 kuhuisha uchumi wao, lakini kuibuka vita vya Ukraine na matukio mbalimbali ambayo yameteteresha uchumi wa dunia, yamelifanya bara hilo kuwa mhanga wa matukio yasiyotarajiwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, licha ya kuweko sera zinazolenga kuhuisha uchumi, lakini inatabiriwa kwamba, ukuaji na ustawi wa uchumi katika mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara utapungua mwaka huu na kufikia 3.6%. Mwakani kiwango hicho kitafikia 3.7% na mwenendo huo wa kupungua utasimama. Aidha malengo ya kiuchumi ya muda mfupi hayana uhakika.
Ripoti zilizotolewa kuhusiana na hasara za kiuchumi zilizosababishwa na janga la virusi vya corona kwa uchumi wa bara la Afrika zinaonyesha kuwa, bara hilo limepata hasara ya dola bilioni 200. Jambo hilo limezifanya nchi nyingi za bara la Afrika kufanya hima ya kuongeza ushirikiano wa kieneo na mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi na mataifa mengine ya dunia, ili kwa njia hiyo yaweze kufidia hasara za kiuchumi zilizosababishwa na msambao wa virusi vya corona.

Katika hali ambayo mataifa ya Afrika yalikuwa mbioni kuhuisha na kuboresha mazingira ya kiuchumi, mara kukaibuka vita vya Ukraine na mgogoro wa nishati uliosababishwa na vita hivyo ni mambo ambayo yamezifanya nchi za Kiafrika kuwa chini ya mashinikizo. Hivi sasa kuna wasiwasi huu kwamba, kuendelea mgogoro wa sasa sambamba na kuwa na taathira hasi kwa miundomsingi ya kiuchumi, kijamii na kiafya ya bara hilo jambo hilo litateteresha pia misingi ya kisiasa ya nchi na bara hilo. Vita vya Ukraine na vikwazo vya madola ya Magharibi dhidi ya Russia vimekwamisha usambazaji wa ngano, mbolea za kemikali na bidhaa nyingine muhimu masuala ambayo yamekuwa na taathira hasi maradufu kwa bara la Afrika.
Raymond Gilpin, mweledi na mwanauchumi mwandamizi anazungumzia mpango wa ustawi na maendeleo wa Umoja wa Mataifa barani Afrika kwa kusema: Huu ni mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa barani Afrika. Hivi sasa tunashuhudia kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa ghafi za ndani barani Afrika.
Takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonyesha kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa wamefikia milioni 193 huku watu milioni 40 wakikabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na usalama wa chakula. Kabla ya kuanza vita, Ukraine ilikuwa moja ya wasambazaji wakuu wa ngano, mahindi na mafuta ya alizeti kwa mataifa mengine ya dunia hususan nchi masikini zaidi za Afrika ya Kaskazini. Russia nayo ina nafasi na mchango muhimu katika kudhamini bidhaa za chakula barani Afrika. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Russia na Ukraine kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa ilikubaliwa kutumwa mafurushi na mizigo ya nafaka mbolea za kemikali katika miezi ya hivi karibuni kwa nchi masikini za Kiafrika. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mizigo hiyo imesafirishwa na kupelekewa nchi tajiri barani Ulaya.
Marlene Timme, Mkuu wa Shirika la Ujerumani la Kusaidia Wenye Njaa Ulimwenguni anasema: Migogoro ya njaa ulimwenguni imekuwa ikiongezeka kutokana na matokeo ya vita.

Hivi sasa nchi za Kiafrika siyo tu kwamba, zimo katika hatari kubwa ya uhaba wa chakula, bali zinakabiliwa na mgogoro wa ukosefu wa ajira. Hii ni katika hali ambayo kutokuwa na natija mipango ya kiuchumi katika akthari ya nchi za bara hilo kumewafanya baadhi ya raia wa nchi hizo kujiunga na makundi yenye kufurutu ada hali ambayo yenyewe inaifanya hali ya mambo katika bara hilo kuwa mbaya.
Inaonekana kuwa, bara la Afrika lingali mhanga mkuu kabisa wa migogoro wa kimataifa na limo katikati ya uwanja wa kupimana misuli madola ya Magharibi katika vita vya Ukraine na kuongezeka mabadiliko ya tabianchi ambayo ni matokeo ya nchi za Magharibi kutofungamana na mikataba ya mazingira na uzalishaji wa hewa chafu na vilevile kuenea ukosefu wa usalama ambao chimbuko lake ni harakati za kigaidi.
David Malpass, Rais wa Benki ya Dunia anasema kuhusiana na hili kwamba: Kwa mpango huu, inaonekana kuwa, malengo ya kimataifa ya kuhitimisha umasikini ifikapo mwaka 2030 kivitendo hayataweza kufikiwa.