Nchi za Afrika zakutana Zanzibar kujadili maji safi na taka
Nchi 42 za Afrika zinakutana Zanzibar nchini Tanzania kuanzia leo kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu udhibiti wa sekta ya maji safi na taka Afrika.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la Tanzania, mkutano huo utakaokuwa na washiriki 150 kutoka kwenye nchi mbalimbali, unaanza leo Jumanne Novemba 15 hadi 18 huko Unguja, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo jana Jumatatu Novemba 14, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Omar Ali Yussuf amesema mkutano huo utahusisha taasisi zote zinazohusiana na udhibiti wa maji Afrika.
Amesema lengo la mkutano ni kuhakikisha kuna mpango maalumu wa kimkakati wa kudhibiti matumizi ya maji baada ya kutumiwa majumbani.
“Tumekuwa na changamoto kubwa kuwa na udhibiti wa maji yaliyotumika, sote ni mashahidi wa miradi mikubwa inayotekelezwa ya maji nchini lakini suala linakuja haya maji yakishatumika yanakwenda wapi,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha miji inakuwa salama na safi, maji yale hayapaswi kusambaa ovyo na kusababisha uchafuzi wa mazingira jambo linaloweza kuleta athari ya maradhi hivyo lazima yadhibitiwe.
Katibu Mkuu Mtendaji wa Umoja wa Wadhibiti wa Maji Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAWAS), Yvonne Magawa amesema mkutano huo utakuwa na maana kubwa kwani ni mara ya kwanza kushiriki nchi zote za Afrika na kanda zake nne.
Mkutano huo utakuwa na kaulimbiu isemayo, 'kuimarisha uwajibikaji kwa sekta husika' ambapo watazungumzia uwajibikaji kwa sababu, mamlaka ndizo zinawajibika kutekeleza sera huku wadhibiti wakiwa wasemaji wakuu wa wananchi.