UN: Raia 160 wameuawa katika mapigano Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umesema raia wasiopungua 166 wameuawa katika mapigano yaliyoshuhudiwa kaskazini mwa Sudan Kusini katika kipindi cha miezi minne iliyopita.
Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa kuwa, mbali na raia 166 kuuawa, wengine zaidi ya 230 wamejeruhiwa katika mapigano hayo baina magenge ya wabeba silaha.
Taarifa ya taasisi hiyo ya UN imeeleza kuwa, maelfu ya watu katika eneo la Upper Nile wamelazimika kutafuta hifadhi kwenye maeneo ya misitu iliyojaa maji wakihofia kuuawa, kubakwa au kutekwa nyara kama walivyofanyiwa wenzao.
Volker Turk, Ofisa Mkuu wa masuala ya haki katika Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema, vita hivyo vimepelekea watu 20,000 wayakimbie makazi yao, ambapo 3,000 miongoni mwao wamekimbilia nchi jirani ya Sudan.

Amesema mapigano hayo yameenea katika majimbo jirani ya Jonglei na Unity, huku raia ziadi ya 1,000 wakikwama katika mji wa Kodok jimboni Upper Nile, wasijue pa kwenda.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini wiki iliyopita alitoa mwito kwa pande hasimu katika mapigano yanayoshuhudiwa nchini humo kuweka silaha chini na kukumbatia amani.