Ghana yaituhumu Burkina Faso kwa kuwaajiri mamluki wa Russia wa "Wagner"
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91780-ghana_yaituhumu_burkina_faso_kwa_kuwaajiri_mamluki_wa_russia_wa_wagner
Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amesema kuwa nchi jirani yake Burkina Faso imeandaa mpango na kundi la wanamgambo wa Russia la "Wagner" ili kuwatumia wanamgambo wa kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2022 23:33 UTC
  • Ghana yaituhumu Burkina Faso kwa kuwaajiri mamluki wa Russia wa

Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amesema kuwa nchi jirani yake Burkina Faso imeandaa mpango na kundi la wanamgambo wa Russia la "Wagner" ili kuwatumia wanamgambo wa kundi hilo.

Rais wa Ghana amesema kuwa, Burkina Faso kama ilivyofanya Mali nayo pia imefikia mapatano ili kulitumia kundi hilo la wanamgambo wa Russia. Ameongeza kuwa, anaamini kwamba wanamgambo hao wametengewa mgodi unaopatikana kusini mwa Burkina Faso kama malipo yao kwa huduma wanazotoa. Nana Akufo-Ado amebainisha hayo katika mkutano na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken. 

Wanamgambo wa Russia wa kundi la "Wagner"

Rais wa Ghana ameendelea kueleza kuwa, mamluki hao wa Wagner wako katika mpaka wa kaskazini wa Ghana; hatua ambayo inatia wasiwasi sana. Akijibu madai hayo ya Rais wa Ghana, Jean-Emmanuel Ouedraogo Msemaji wa serikali ya Burkina Faso ameeleza na hapa ninamnukuu: "hatuna majibu. Ninamwachia jukumu la kile alichosema".

Itakumbukwa kuwa, katika nchi kadhaa za Kiafrika zinazozungumza lugha ya Kifaransa, Russia inaendesha kampeni athirifu khususan katika  mitandao ya kijamii  sambamba na kuongezeka  uungaji mkono mkubwa wa nchi hiyo huku  ushawishi wa Ufaransa ukizidi kupungua katika nchi hizo. 

Hii ni katika hali ambayo nchi kadhaa zinaikosoa serikali ya kijeshi iliyoko madarakani huko Mali kwa kuwa karibu na kundi la wanamgambo wa Russia la Wagner. Serikali hiyo inadaiwa  kuwa karibu na serikali ya Moscow; madai ambayo yamekanushwa na Mali.