Mgomo mkubwa Tunisia; jibu la kutotekeleza ahadi Rais Kais Saied
Muungano Sekta ya Usafiri na Uchukuzi wenye mfungamano na Muungano Mkubwa wa Wafanyakazi nchini Tunisia (UGTT) umetangaza mkakati wake wa kufanya mgomo wa siku mbili Januari 25 na 26 mwaka 2023.
Muungano Mkuu wa Wafanyakazi Tunisia umesema kuwa, utatekeleza mgomo huo wa siku mbili lengo likiwa ni kukemea hatua ya serikali ya kuyaweka kando makampuni ya umma na kupuuzwa hali mbaya inayoyakabili makampuni hayo. Mgomo huo unatazamiwa kusababisha usumbufu mkubwa kwa upande wa huduma za usafiri, ikiwa ni pamoja na usafiri wa anga, ardhini, baharini na usafirishaji wa mizigo.
Aidha maandamano yanatazamiwa kufanyika sambamba na mgomo huo tajwa wa mwezi Januari katika maidani za katikati ya miji na katika maeneo ya umma nje ya ofisi za serikali.
Mgomo katika sekta ya usafiri na uchukuzi unatarajiwa kufanyika kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zake Rais Kais Saied wa nchi hiyo kuhusiana na kuinasua nchi hiyo kutoka katika mgogoro wa kisiasa na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hapana shaka kuwa, huo ni mlolongo wa malalamiko ya wananchi wa Tunisia dhidi ya siasa na sera za Rais Kais Saied.
Mnamo Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya Wabunge, kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha al-Nahdha.
Kabla ya hapo pia, kumewahi kufanyika mgomo mkubwa wa nchi nzima nchini Tunisia. Juni mwaka huu pia, wafanyakazi wa sekta ya umma nchini Tunisia waliitisha mgomo mkubwa kulalamikia mgogoro wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo na hali mbaya ya maisha inayowakabili wananchi wa nchhi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kutoa wito wa kuboreshwa hali ya kazi na maisha kiujumla. Jumla ya jumuiya 159 zikiwemo idara za serikali, bandari na viwanja vya ndege ziliitikia mwito huo wa kushiriki katika mgomo huo ambapo takwa lao kuu lilikuwa ni kuongezwa mishahara ili uwezo wao wa kununua uongezeke hasa kwa kuzingatia kuweko mgogoro wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa.
Ukweli wa mambo ni kuwa, licha ya ahadi nyingi alizotoa Rais Kais Saied, lakini hadi sasa ameshindwa kutekeleza ahadi hizo na kumfanya akalie kuti kavu.
Julai 25, mwaka huu, Kais Saeid aliitisha kura ya maoni ya katiba mpya ambayo ilipitishwa licha ya kupigiwa kura na Watunisia wachache, ambapo kiwango cha ushiriki katika kura hiyo ya maoni kilitajwa kuwa ni asilimia 27.5. Ushiriki huo wenyewe ulikuwa ni ishara ya wazi ya wananchi wa nchi hiyo ya kulalamikia maamuzi ya Rais Kais Saied.
Wapinzani wanachukulia hatua za Rais wa Tunisia kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba iliyoidhinishwa mwaka 2014 na mabadiliko ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa Zine El Abidine Ben Ali, lakini Saied mwenyewe anasisitiza kuwa, hatua zake zimelenga kuiokoa Tunisia na msambaratiko wa kiuchumi na kijamii. Katika hatua iliyofuata, Rais wa Tunisia alitangaza kufanya mabadiliko katika sheria za uchaguzi ambapo alidai kuwa, lengo la mabadiliko hayo ni kuzuia ukiukaji wa sheria na maagizo ya kuwachagua Wabunge fulani na vilevile kuzuia kuenea fedha za ufisadi. Miongoni mwa yaliyomo katika sheria mpya za uchaguzi ni kupunguzwa idadi ya viti vya Bunge kutoka 217 na kuwa 161.
Pamoja na hayo yote, ushiriki mdogo wa wananchi wa Tunisia katika uchaguzi wa Bunge wa mara hii ni ishara ya wazi kwamba, wananchi wa nchi hiyo hawana imani tena na Rais Kais Saied, kaulimbiu na hata ahadi zake. Baada ya kuingia madarakani Rais huyo alidai kwamba, mageuzi yake yatalenga kupambana na ufisadi, mkwamo wa kisiasa na mdodoro wa kiuchumi. Awali hatua zake zilipokelewa vizuri na baadhi ya wananchi. Hata hivyo kuendelea hatua na juhudi zake za kuhodhi madaraka, kuzisambaratisha na kuzibinya asasi za kisheria na kutotekeleza ahadi zake ni mambo yaliyopelekea kupungua kupendwa kwake na hata uungaji mkono wa wananchi kwa kiongozi huyo.
Baada ya ushiriki mdogo wa wananchhi katika uchaguzi wa bunge hivi karibuni, Nejib Chebbi, kiongozi wa Muungano wa Uokovu alimtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo ajiuzulu kutokana na ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi wa bunge na kubainishha kwamba, kilichotokea katika uchaguzi huo ni mithili ya zilzala katika medani ya kisiasa ya Tunisia ambayo itakuja na mabadiliko makubwa.