Rais wa Somalia awataka raia wawafurushe 'kunguni' wa al-Shabaab
Rais wa Somalia ametoa mwito kwa raia wa nchi hiyo waunge mkono jitihada za vyombo vya usalama za kupambana na ugaidi kwa kuwatimua wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab aliowataja kuwa 'makunguni'.
Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema hayo akihutubia umati wa wananchi wa Somalia waliokusanyika katika uwanja mmoja huko Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, raia wa kawaida wana wajibu wa kuunga mkono juhudi za kulitokomeza kundi hilo.
Rais Mohamud amebainisha kuwa, "Natoa mwito kwenu, wakazi wa Mogadishu, kuwatimua hawa Makhawarij ambao wapo miongoni mwenu. Wanaishi katika majumba yenu, ni majirani zenu, wapo ndani ya magari yanayowapita, wafurusheni."
Rais wa Somalia ameongeza kuwa, "Wanachama wa al-Shabaab ni kama kunguni waliojificha katika nguo zenu, wananchi wamechoshwa na mauaji ya halaiki na vitendo vingine viovu wanavyovifanya, wanasema imetosha sasa."
Hadhirina waliokusanyika kusikiliza hotuba ya Rais wa Somalia walikuwa wamebeba bendera ya nchi hiyo na mabango yaliyokuwa na jumbe za kulaani jinai za kundi la kitakfiri la al-Shabaab linaloua raia, maafisa wa serikali na maafisa usalama wa nchi hiyo na jirani.
Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Somalia kutangaza kwamba, genge hilo la kigaidi limeomba kufanya mazungumzo nayo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa magaidi hao kuomba kukutana na kuzungumza na serikali ya Mogadishu.
Hii ni katika hali ambayo, vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya Pembe ya Afya vimeshadidisha operesheni zao dhidi ya wanamgambo hao, na hivi karibuni, viliangamiza magaidi 61 wa genge hilo katika mkoa wa Shabelle ya Kati, kusini mwa nchi.