AU: Tunaridhishwa na mafanikio ya SNA katika vita dhidi ya al-Shabaab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i93060-au_tunaridhishwa_na_mafanikio_ya_sna_katika_vita_dhidi_ya_al_shabaab
Umoja wa Afrika umesema kwamba umetiwa matumaini na stratejia inayotumia na Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) katika operesheni zake za kulisambaratisha kundi la kigaidi la al-Shabaab, haswa kwa kutilia maanani mafanikio makubwa liliyoyapata katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 19, 2023 10:19 UTC
  • AU: Tunaridhishwa na mafanikio ya SNA katika vita dhidi ya al-Shabaab

Umoja wa Afrika umesema kwamba umetiwa matumaini na stratejia inayotumia na Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) katika operesheni zake za kulisambaratisha kundi la kigaidi la al-Shabaab, haswa kwa kutilia maanani mafanikio makubwa liliyoyapata katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Balozi Mohammed al-Amin Souef, Mkuu wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) amesema wamefurahishwa na hatua zilizopigwa mpaka sasa na SNA, na kwamba wanatumai kuwa, katika mustakabali wa karibuni, genge hilo la wanamgambo litasambaratishwa kikamilifu nchini Somalia.

Sambamba na kuvipongeza vikosi vya serikali ya Somalia kwa kufanikiwa kukomboa miji kadhaa ya kistratejia katika siku za hivi karibuni, Balozi Souef amesisitiza kuwa, AU itaendelea kuipa Somalia msaada na uungaji mkono unaohitajika ili taifa hilo la Pembe ya Afrika liondokane na ugaidi na vitendo vinavyohusiana nao.

Katika muda wa wiki moja iliyopita pekee, Jeshi la limefanikiwa kukomboa miji kadhaa toka mikononi mwa wapiganaji wa al-Shabaab, ikiwemo El-Dheer, Harardhere, Galcag na Hindheere katika majimbo ya Galmudug na Galgadud, katikati ya nchi.

Wanajeshi wa kulinda amani wa AU nchini Somalia

Kabla ya hapo, vikosi hivyo viliukomboa mji mwingine wa Runirgoud, ngome ya mwisho ya magaidi hao wakufurishaji huko Shabelle ya Kati, takriban kilomita 240 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu. 

Al-Shabaab imepoteza sehemu kubwa ya maeneo iliyokuwa inayakaliwa kwa mabavu tangu Agosti mwaka jana, wakati vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na wanamgambo wa koo vilipoanzisha operesheni kusini na katikati mwa Somalia.

Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kuhusishwa kwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ambao ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na magaidi wa al-Shabaab.