Jan 29, 2023 12:28 UTC
  • Ushiriki mdogo watazamiwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge Tunisia

Idadi ndogo ya wapiga kura wanatazamiwa kushiriki duru ya pili uchaguzi wa Bunge nchini Tunisia wa leo, baada ya makundi ya upinzani kikiwemo chama cha Kiislamu chenye ushawishi mkubwa nchini humo cha Annahdha kutoa miito ya kususia uchaguzi huo.

Wagombea 262 wakiwemo wanawake 34 wanachuana katika zoezi hilo la kidemokrasia la kuwachagua Wabunge 131 kati ya 161 wa Bunge la nchi hiyo, ambalo limepokonywa sehemu kubwa ya mamlaka yake, tangu Rais Kais Saied wa nchi hiyo aanzishe wimbi la hatua za kutwaa madaraka ya nchi hiyo mnamo Julai 25, 2021.

Wachambuzi wa mambo wanasema aghalabu ya wananchi wa Tunisia ambao wamezongwa na matatizo ya kiuchumi, ughali wa maisha na mfumko wa bei huenda hawatashiriki zoezi hilo. 

Youssef Cherif, Mkurugenzi wa taasisi ya Columbia Global Centers amesema, "Bunge halitakuwa na uhalali kamili, kwa kuwa Rais ambaye alitwaa madaraka yote ya nchi kufuatia kura ya maoni ya Katiba mwaka 2022, atalidhibiti (Bunge hilo) kikamilifu." 

Ikumbukwe kuwa, akthari ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura nchini Tunisia walisusia duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika mnamo Disemba 17 mwaka uliopita 2022.

Rais Kais Saied

Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia ilitangaza kuwa, ni asilimia 11 tu ya wapiga kura milioni 9.2 walioshiriki zoezi hilo la uchaguzi wa Bunge nchini humo mwaka uliopita. Wagombea 23 walichaguliwa katika uchaguzi huo.

Hii ni katika hali ambayo asilimia 40 ya wananchi wa Tunisia waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katika uchaguzi uliopita wa Bunge wa mwaka 2019. Vyama vya upinzani nchini Tunisia vinasema, Rais Kais Saied amepoteza uhalali wa kuendelea kuwa kiongozi wa nchi hiyo, baada ya Watunisia wengi kususia uchaguzi huo.

Tags