Jan 31, 2023 06:53 UTC
  • Watu 30 wapoteza maisha kutokana na kimbunga cha tropiki Madagascar

Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na kimbunga kikali cha tropiki cha Cheneso kilichoipiga Madagascar imeongezeka na kufikia 30.

Hayo yalisemwa jana Jumatatu na Ofisi ya Taifa ya Kudhibiti Hatari na Majanga ya nchi hiyo, (BNGRC) iliyoeleza kuwa, mbali na watu 30 kuthibitishwa kuaga dunia kwenye janga hilo la kimaumbile, wengine zaidi ya 20 wametoweka.

Taarifa ya ofisi hiyo imeongeza kuwa, watu 89,000 wameathiriwa na kimbunga hicho katika mikoa 15; kati yao, watu 23,600  wamehamishwa. Taarifa hiyo pia imesema, maji yamefurika kwenye nyumba 13,356 huku nyumba nyingine 500 zikiharibiwa kabisa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, kimbunga cha Cheneso kilitua Januari 19 kwenye pwani ya kaskazini mashariki mwa nchi ya kisiwa cha Bahari ya Hindi na kuelekea kusini-magharibi.

Athari za kimbunga Madagascar

Mbali na mafuriko hayo, Ofisi ya Taifa ya Kushughulikia Maafa na Majanga ya Kimaumbile ya Madagascar imesajili matukio kadhaa ya maporomo ya udongo. 

Vimbunga vimekuwa vikiikumbwa Madagascar mara kwa mara, ambavyo husababisha maafa makubwa ya roho na mali. Malaki ya watu wamekuwa wakiacha bila makazi, huku miundombinu na mifumo ya mawasiliano ikiharibiwa vibaya.

Tags