Guinea ya Ikweta imesajili mripuko wa kwanza wa Marbug, WHO
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Equatorial Guinea imethibitisha habari ya kukumbwa na mripuko wa kwanza wa ugonjwa wa virusi vya Marburg.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na WHO inasema kuwa, kwa akali watu tisa wamethibitishwa kufariki dunia nchini humo kutokana na virusi hivyo vinavyoua kwa haraka kama virusi vya Ebola.
Aidha kesi 16 zinazoshukiwa kuwa za maradhi hayo zimesajiliwa katika mripuko huo, hali ambayo imezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia wa nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi.
Ugonjwa huo unaoua haraka kama Ebola husababisha mgonjwa kutokwa na damu, kutapika na kuharisha na ni ugonjwa wenye kuambukiza haraka.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa limetuma maafisa wake nchini Guinea ya Ikweta ili kuimarisha juhudi za kuzuia maambukizi zaidi ya homa hiyo.

Ikumbukwe kuwa, mnamo Agosti mwaka 2021, Shirika la Afya Duniani lilitangaza habari ya kusajiliwa kesi ya kwanza ya kifo kilichosababishwa na virusi hatari vya Marburg nchini Guinea huko Magharibi mwa Afrika.
Virusi vya Marburg vinaweza kumuua mtu mwenye afya katika kipindi cha wiki moja tu baada ya kuanza kutapika na kuharisha na hatimaye kutokwa damu ndani kwa ndani. Ugonjwa huo hauna tiba.