Tinubu wa chama tawala Nigeria atangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais
Mgombea wa chama tawala nchini Nigeria, Bola Tinubu ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi iliyopita.
Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) imemtangaza Tinubu aliyegombea kupitia chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kuwa mshindi wa uchaguzi urais, kwa kuzoa kura milioni 8.8, akifuatiwa na mshindani wake wa karibu Atiku Abubakar wa chama cha Peoples Democratic Party (PDP) aliyeambulia kura milioni 6.9.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi Nigeria, mgombea wa Chama cha Leba, Peter Obi, ameibuka wa tatu kwa kupata kura milioni 6.1 katika uchaguzi huo wa kutafuta mrithi wa Muhammadu Buhari aliyemaliza uongozi wake wa mihula miwili.
Mahmood Yakubu, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) amemtangaza Tinubu anayefahamika kwa jina la utani kama 'Jagaban' kuwa mshindi halali wa uchaguzi wa urais. Amesema mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 70 na ambaye amewahi kuwa Gavana wa jimbo la Lagos baina ya mwaka 1999 na 2007 amepata kura 8,805,420.
Kwa mujibu wa tume hiyo, mbali na kupata kura nyingi zaidi, Tinubu amefanikiwa kuvuka kiunzi cha pili, cha kutakiwa kuzoa asilimia 25 ya kura katika majimbo 25 kati ya 36 ya nchi hiyo, kama ilivyoanishwa kwenye Kipengee cha 134 cha Katiba ya Nigeria.
Hii ni katika hali ambayo, mapema jana, mwakilishi wa PDP katika kituo cha uchaguzi huko Abuja alielezea mchakato huo kuwa wa udanganyifu, na kushutumu chama tawala cha APC kuwa kinashirikiana na INEC, huku chama cha Labour kikiomba kusitishwa matangazo hayo, au uchaguzi kufutwa na kurudiwa upya.
Huku hayo yakijiri, Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye anaongoza timu ya uangalizi ya Umoja wa Afrika kwenye uchaguzi huo amewataka viongozi ambao hawajaridhishwa na mchakato wa zoezi hilo la kidemokrasia kufuata sheria kwa kuwasilisha malalamiko yao mahakamani.
Wakati huo huo rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ameitaka Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kuiokoa nchi kutokana na "hatari inayokuja" kutokana na kile alichokitaja kuwa ufisadi wa mchakato wa uchaguzi. Vilevile Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya umekosoa ukosefu wa uwazi na utendaji mbaya katika uchaguzi wa Nigeria, kulingana na matokeo yake ya awali.