Rais Ruto: Kenya haitaruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja
Rais William Ruto wa Kenya amekosoa uamuzi wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo wa kuruhusu kusajiliwa makundi ya kulobi ya mashoga na wasagaji (LGBTQ) na kusisitiza kuwa, taifa hilo la Afrika Mashariki kamwe halitaruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja.
Rais Ruto alisema hayo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, Kenya haitaruhusu kuenea vitendo vya kifuska vya ushoga, ambavyo vinakinzana na mafundisho ya dini na tamaduni za Kiafrika.
Dakta Ruto amesema, "Mimi ni mtu wa Mungu, ingawaje tunaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu, lakini dini na tamaduni zetu haziruhusu mwanamke kuolewa na mwanamke au mwanaume kumuoa mwanaume mwenzake."
Rais Ruto amesisitiza kuwa, uozo huo wa ushoga na usagaji unaweza kufanyika kwengineko duniani lakini si katika ardhi ya Kenya. Amesema, "Hatuwezi kwenda mabarabarani kushinikiza (mashoga na wasagaji) waoane hapa nchini."
Naye Naibu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema binafsi ameshtushwa na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu wa kuruhusu kusajiliwa makundi ya mashoga nchini humo.
Kwa upande wake, kinara wa upinzani nchini humo, Raila Odinga amekashifu uamuzi huo wa Mahakama ya Kilele nchini humo na kueleza kuwa, kazi ya mhimili huo wa serikali ni kufafanua na kutoa maelezo juu ya sheria, lakini si kutunga sheria.
Odinga amesema, "Kipengee cha 45:2 cha Katiba ya Kenya kinasema wazi kuwa, mtu mzima ana haki ya kuoa (kuolewa) na mwenzake wa jinsia tofauti."