WHO: Nchi 37 za Afrika zinakabiliwa na uhaba wa wahudumu wa afya
(last modified Wed, 15 Mar 2023 12:11:05 GMT )
Mar 15, 2023 12:11 UTC
  • WHO: Nchi 37 za Afrika zinakabiliwa na uhaba wa wahudumu wa afya

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema nchi 37 za bara Afrika zinakabiliwa na hatari kutokana na uhaba wa wahudumu wa afya.

WHO imesema mifumo ya afya ya nchi hizo inabailiwa na mtikisiko kwa kuwa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanaondoka katika nchi hizo na kwenda kutafuta ajira ughaibuni.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kwa ujumla nchi 55 duniani zikiwemo 37 za Afrika zinakabiliwa na hatari kutokana na uhaba wa wahudumu wa afya.

Taarifa ya WHO iliyotolewa jana Jumanne imesema kuwa, mbali na nchi 37 za Kiafrika, nyingine 8 zinazokodolewa macho na hatari ya afya ni za eneo la Pasifiki Magharibi, 6 za eneo la Mashariki mwa Mediterrania, 3 za Kusini Mashariki mwa Asia na moja ya kanda ya Amerika.

Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema wahudumu wa afya ni uti wa mgongo wa mfumo wowote ule wa afya, na kwamba uhaba wa madaktari na wahudumu wa afya katika nchi hizo unawasababishia matatizo raia wa mataifa hayo.

Mgomo na maandamano ya madaktari nchini Kenya

Kwa mfano, Nigeria, nchi yenye zaidi ya watu milioni 220, ina madaktari 10,000 pekee, suala ambalo linawafanya wagonjwa wakabiliwe na matatizo mengi katika kupata huduma za matibabu.

Aidha Uingereza ambayo hivi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wauguzi na walimu baada ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, imekuwa ikijielekeza katika koloni lake la zamani, Zimbabwe kutafuta wafanyakazi wa sekta hizo.