Je, Iran na nchi za Afrika zinawezaje kukamilishana kiuchumi?
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa serikali ya Iran inalipa kipaumbele maalumu suala la mahusiano na bara la Afrika, na ameonesha matumaini ya mustakabali mwema katika ushirikiano wa pande mbili.
Akizungumza Jumapili usiku katika hafla ya kuadhimisha miaka 62 ya Umoja wa Afrika mjini Tehran, Waziri Araghchi amelisifu bara la Afrika kwa historia yake ya kupinga ukoloni na kusisitiza mshikamano wa muda mrefu uliopo kati ya Iran na bara hili. Amesema kuwa Iran inatafuta fursa za ushirikiano wa kiuchumi na nchi za Afrika katika muktadha wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA)
Hafla hiyo, iliyobeba kaulimbiu ya “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia,” ilihudhuriwa na mabalozi kadhaa wa nchi za Afrika pamoja na Waafrika walioko Tehran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, kutokana na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Iran na Afrika, Iran inatafuta ushirikiano wa kiuchumi ndani ya mfumo wa AfCFTA na kupitia ushirikiano wa nchi na nchi, kwa imani kuwa Iran na mataifa ya Afrika yanaweza kukamilishana katika nyanja hii na kuimarisha uhusiano wao wa karne nyingi.
Waziri huyo ameeleza kuwa, wingi wa rasilimali asilia barani Afrika pamoja na uwezo wa Iran katika teknolojia ya kisasa vinatoa jibu muafaka kwa mahitaji ya pande zote mbili. Amesema kuwa kufanikiwa kwa duru ya tatu ya Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika lililofanyika mwezi uliopita ambalo liliungwa mkono kwa dhati na viongozi wa ngazi za juu wa Afrika, ni ishara njema ya mustakabali wa kupanua ushirikiano baina ya pande hizi mbili, ambao utazidi kuimarika kupitia mikutano ijayo.
Hali kadhalika Araghchi amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa bega kwa bega na Afrika kama rafiki wa kweli wa muda mrefu. Amesema: “Sasa, zaidi ya nusu karne tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizi mbili, tunapaswa kuchukua hatua stahiki kuhakikisha uhusiano huu unadumu." Ameongeza kuwa: "Muungano wa Kusini mwa Dunia (Global South), kwa kuzindua mpango mpya na utaratibu mpya, unaonesha hatima ya pamoja na udugu katika njia ya maendeleo na ustawi.”

Katika upande mwingine, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ujumbe wake uliochapishwa katika mtandao wa X, imetoa pongezi kwa mnasaba wa Siku ya Afrika na kuichukulia siku hii kuwa ukumbusho wa juhudi za mshikamano na ushirikiano baina ya mataifa ya Afrika. Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ulianzishwa tarehe 25 Mei, 1963.
Bara la Afrika, pamoja na kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, linaweza kuchukuliwa kuwa mshirika mzuri wa Iran kwa mtazamo wa kiuchumi, na kwa mtazamo wa kisiasa, linaweza pia kuwa na nafasi ya kuiunga mkono Iran katika taasisi na majukwaa ya kieneo na kimataifa, jambo ambalo linaweza kufikiwa kwa kuzingatia hali ya pamoja kati ya pande hizo mbili.
Muelekeo wa kisiasa wa uhusiano na nchi za bara la Afrika pia ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nchi za Kiafrika zinaunda thuluthi moja ya nchi za dunia, hivyo kuenezwa uhusiano na nchi hizo kunaweza kutoa msingi zaidi wa uungaji mkono wa kimataifa kwa Iran ambayo iko chini ya vikwazo haramu vya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.
Pia inapaswa kukumbwa kwamba, kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara la Afriak na karibu 50% ya wakazi wake ni Waislamu; Pia, nchi 50 kati ya 54 za bara hili ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).
Kwa kupanua uhusiano wa kiuchumi na bara la Afrika, Iran inaweza kuunda fursa za kiuchumi na nchi za Kiafrika na kubadilisha washirika wake wa kibiashara na kutoa bidhaa, huduma na teknolojia zake kwa soko hili. Iran inataka kupunguza utegemezi kwa masoko ya Ulaya na Marekani, na kupanua uhusiano na nchi zisizo za Kimagharibi.

Bara la Afrika pia lina akiba kubwa ya mafuta, gesi, dhahabu, almasi, urani na madini mengine, na Iran inaweza kupata rasilimali hizi kupitia ushirikiano wa kiufundi na uwekezaji wa pamoja. Kustawi uhusiano wa kiuchumi wa Iran na nchi za Kiafrika kunaweza pia kupelekea kuimarishwa ushirikiano wa kisiasa na kiusalama na nchi za bara hilo tajiri.
Iran inaweza kushiriki katika miradi ya Kiafrika katika nyanja kama vile nishati, kilimo, viwanda na teknolojia, na makampuni ya Iran yana uwezo mkubwa wa kujenga barabara, viwanda vya kusafisha mitambo, mitambo ya kuzalisha umeme na miradi ya maji.
Ushirikiano wa Iran na nchi za bara la Afrika ni muhimu kiuchumi (upatikanaji wa masoko na rasilimali) na kisiasa (kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi na kupanua ushawishi). Uhusiano huu unaweza kupelekea ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili na kuimarisha nafasi ya kimataifa ya Iran.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kupanuliwa uhusiano kati ya Iran na nchi za Kiafrika pia kuna umuhimu wa kisiasa na kiutamaduni. Uwezo wa kisayansi na kiufundi wa Iran katika kutoa huduma na uwekezaji katika bara la Afrika ni miongoni mwa mipango ya muda mrefu ya Iran ya kuwepo katika bara la Afrika.