Mar 16, 2023 10:00 UTC
  • Baraza la Usalama laongeza muda wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha uamuzi wa kuongezea muda wa Operesheni Maalumu ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) kwa mwaka mmoja, hadi tarehe 15, Machi mwaka 2024.

Nchi 13 wanachama wa Baraza la Usalama jana Jumatano zilipiga kura ya kuunga mkono uamuzi huo wa kurefushwa muda wa kuhudumu vikosi vya UNMISS nchini Sudan Kusini, huku Russia na China zikijizuia kupiga kura.

Taarifa ya UN imesema kuwa, operesheni ya timu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) inayojumuisha wanajeshi 17,000 na maafisa wa polisi  2,101 ni moja ya operesheni zenye gharama kubwa zaidi za UN, na hutengewa bajeti ya dola bilioni 1.2 kila mwaka.

Umoja wa Mataifa umezitaka pande mbalimbali za Sudan Kusini zisimamishe vita mara moja, na kusema Baraza la Usalama linatafakari suala la kuchukua hatua za kuwaadhibu watu wanaovuruga amani, utulivu na usalama wa Sudan Kusini.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Rais Salva Kiir (kushoto) na Makamu wake, Riek Machar

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Baraza la Usalama limeongeza muda wa vikosi vya kulinda amani Sudan Kusini wakati huu ambapo mzozo unaonekana kuibuka tena katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, baina ya Rais Kiir na makamu wake Riek Machar juu ya mabadiliko ya kushtukiza yaliyofanywa mwezi huu kwenye baraza la mawaziri.

Tags