Waungaji mkono wa Rais wa Tunisia waandamana dhidi ya 'wasaliti'
Mamia ya wafuasi wa serikali ya Rais Kais Saied wa Tunisia jana Jumatatu walifanya maandamano katika mji mkuu Tunis, kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo anayekabiliwa na mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu.
Waandamanaji hao wamewaonya vikali raia wa nchi hiyo wanaofanya maandamano dhidi ya serikali na kuwataja kuwa wasaliti, huku wakiwakosoa wanadiplomasia wa nchi za kigeni wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Lobna Souissi, mmoja wa waandamanaji hao amesema "Tunamuunga mkono (Rais) Saied kwa kampeni yake dhidi ya wasaliti na mafisadi, na vile vile tunasimama dhidi ya uingiliaji wa kigeni."
Baadhi ya watu waliokamatwa katika siku za hivi karibuni kwa kufanya maandamano dhidi ya serikali, wanatuhumiwa kukutana na kufanya mawasiliano na wanadiplomasia wa Marekani na Ufaransa nchini humo.
Waandamanaji hao wametoa mwito kwa wanadiplomasia wa nchi ajinabi walioko nchini humo kuheshimu Hati ya Vienna Kuhusu Mahusiano ya Kigeni, inayowataka waheshimu sheria za nchi walikotumwa, na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi husika.
Haya yanajiri siku chache baada ya mrengo mkubwa zaidi wa upinzani huko Tunisia kufanya maandamano ya kutaka kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa sambamba na kumtaka Rais Kais Saied ajiuzulu.
Maandamano hayo ya waungaji mkono kwa upande mmoja na wapinzani wa serikali kwa upande mwingine yanafanyika huku kukiwa na mzozo mkubwa wa kisiasa ambao ulizidisha hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo tangu 2021 wakati Rais wa Tunisia Kais Saied alipovunja bunge na kutwaa mamlaka yote ya utendaji.