Zimbabwe kujinaisha kuajiriwa wafanyakazi wake wa afya katika nchi za kigeni
(last modified Fri, 07 Apr 2023 02:21:30 GMT )
Apr 07, 2023 02:21 UTC
  • Zimbabwe kujinaisha kuajiriwa wafanyakazi wake wa afya katika nchi za kigeni

Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga, ametangaza kuwa nchi hiyo inakusudia kuanzisha sheria ambayo itafanya kuwa kinyume cha sheria kwa mataifa mengine kuajiri wafanyikazi wake wa afya.

Zimbabwe imesema hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kuzuia upotevu wa wataalamu wa afya wa nchi hiyo wenye thamani wanaokimbilia katika nchi mbalimbali, jambo ambalo limekuwa likitukia mara kwa mara katika mfumo wa afya wa Zimbabwe.

Makamu wa Rais wa Zimbabwe ambaye pia ni Waziri wa Afya wa nchi hiyo ameeleza kuwa kitendo cha nchi kukosa wataalamu wa afya kwa kukimbilia katika nchi za nje ni sawa na kufanya biashara ya binadamu.

Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Zimbabwe ametangaza adhabu kali kwa wale wote ambao amedai kuwa walilikosesha taifa hilo mtaji wa nguvu kazi ya rasilimali watu. 

Constantino Chiwenga ameeleza kuwa, iwapo mtu kwa makusudi, ataajiriwa na kuisababishia nchi matatizo, basi kitendo hicho kitahesabiwa kuwa jinai dhidi ya binadamu. Amesema, hivi sasa watu wanakufa mahospitalini kwa sababu hakuna wauguzi na madaktari, na jambo hili lazima lishughulikiwe kwa uzito wa hali wa juu." 

Zimbabwe yakabiliwa na upungufu wa wauguzi na madaktari 

Takwimu zinaonyesha kuwa  wauguzi na madaktari zaidi ya 4,000 wameondoka Zimbabwe tangu Februari mwaka 2021. Sekta ya  Afya  ya Taifa ya Uingereza imekuwa kituo cha kuvutia madaktari na wauguzi kutoka Zimbabwe kwa sababu mishahara ni mikubwa zaidi kuliko ile wanayolipwa nyumbani. 

Chama cha Madaktari wa Zimbabwe kimetangaza kuwa nchi hiyo ina jumla ya madaktari wasiopungua 3,500 mkabala wa jamii ya watu milioni 15.