Makumi watiwa nguvuni Ethiopia baada ya mauaji ya afisa wa chama tawala
(last modified Mon, 01 May 2023 07:10:13 GMT )
May 01, 2023 07:10 UTC
  • Makumi watiwa nguvuni Ethiopia baada ya mauaji ya afisa wa chama tawala

Askari usalama wa Ethiopia wametangaza kuwa wamewakamata watu 47 kufuatia mauaji ya afisa wa chama tawala nchini humo.

Askari usalama wa Ethiopia walitangaza Jumapili kwamba, Grima Yeshitila, mkuu wa kieneo wa chama chenye uhusiano na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, na watu wengine 4 waliuawa katika shambulio lililotokea Kaskazini mwa Ethiopia.

Taarifa iliyotolewa na askari usalama wa Ethiopia imesema, watu waliotekeleza mauaji hayo wanatuhumiwa kwa vitendo vya ugaidi na wote walikuwa na silaha, mabomu na vifaa vya mawasiliano ya satelaiti.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa, washukiwa hao wa Kaskazini mwa Ethiopia na nchi nyingine wameshirikiana kwa shabaha ya kudhibiti serikali ya eneo hilo ili kuiangusha serikali kuu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed hivi karibuni alitangaza katika taarifa yake kwamba serikali ya Ethiopia inakusudia kukomesha harakati za makundi yenye silaha na kuyaingiza katika jeshi la taifa.