"Yesu wa Tongaren" afikishwa mahakamani nchini Kenya
-
"Yesu wa Tongaren"
Raia wa Kenya aliyejitangaza kuwa ni Yesu na kuanzisha Kanisa la New Jerusalem eneo la Tongaren, Bungoma, alitarajiwa kurejeshwa mahakamani leo Ijumaa baada ya kulala kwenye seli ya polisi.
Bw Eliud Wekesa atazamiwa kufikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Bw Tom Mark Orlando, ili kuamua iwapo atawaruhusu polisi kumfanyia uchunguzi wa kiakili au la.
Hatua hii inakuja wakati serikali ya Kenya ikiwa mbioni kuwadhibiti wahubiri wenye msimamo na itikadi kali wa Kikristo.
Polisi kupitia Mkurugenzi wa DCI Kaunti ya Bungoma, Bw Elijah Macharia, wasema huenda Bw Wekesa alirukwa na akili.
Polisi wanaamini mtu mwenye akili timamu hawezi kuamka tu na kujifanya ni Yesu Kristo, ambaye waumini wa Ukristo na Waislamu wanaamini atarejea tena duniani.
Kwa sababu hiyo, waliomba mahakama iwaruhusu kumzuilia mshukiwa kwa siku saba, na itoe kibali cha kumpima akili. Polisi pia waliomba kibali cha kwenda kufanya upekuzi katika makazi ya mhubiri huyo, pamoja na eneo lake la kuabudia.
Walidai endapo mshukiwa ataachiliwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa ataingilia na kutatiza uchunguzi.
Wekesa alifikishwa kortini kwa mara ya kwanza jana Alhamisi baada ya kuhojiwa tangu Jumanne.
Polisi wanamtuhumu kuendesha madhehebu yenye itikadi kali eneo la Tongaren, akijidai kuwa ndiye “Masihi”.
Wanasema kwamba anawapa wafuasi wake wakiwemo watoto, mafunzo tatanishi na anaendeleza utakasaji pesa zinazopatikana kwa njia haramu.
Kutokana na kukithiri visa na mikasa inayosababishwa na wachungaji wa Kikristo, Rais William Ruto wa Kenya hivi karibuni aliteua kikosi kazi cha kutathmini kanuni zinazosimamia taasisi za kidini nchini humo.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kuripotiwa vifo vya makumi ya wafuasi wa kanisa la Good News International linaloongozwa mhubiri wa Kikrsito, Paul Mackenzie, ambaye wafuasi wake wanasema alitabiri mwisho wa dunia ungekuwa tarehe 15 Aprili na hivyo kuwaagiza kujiua ili wawe wa kwanza kwenda mbinguni na kukutana na Yesu.

Polisi ya Kenya inasema, idadi ya walioaga dunia kutokana na imani potofu za mchungaji huyo imefika watu 150 huku idadi ya wale waliookolewa wakiwa hai ikifikia 72.
Idadi hiyo ilitangazwa jana Alkhamisi katika siku ya tatu ya awamu ya pili ya ufukuaji wa makaburi ili kutoa miili ya watu waliozikwa kwenye msitu wa Shakahola Kaunti ya Kilifi, baada ya kufukua makaburi katika shamba linalodaiwa kuwa la mhubiri Paul Mackenzie.