Mgombea urais wa muungano wa wapinzani DRC atuhumiwa kufanya wizi
Mgombea urais wa muungano wa wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametuhumiwa kupora nyumba ya raia mmoja wa Ubelgiji.
Mwendesha mashtaka wa mji wa Lubumbashi katika mkoa wa Haut-Katanga wa kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemtuhumu Moise Katumbi, mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa wapinzani wa serikali ya DRC kuwa amefanya uporaji wa nyumba ya raia wa Ubelgiji ajulikanaye kwa jina la Alexandros Stoupis na baadaye kuiuza.
Viongozi wa Kongo wameitaka mahakama imuhukumu kifungo cha miaka mitano jela, mgombea huyo wa urais wa muungano wa wapinzani.
Hata hivyo mawakili wa Moise Katumbi hawakupewa nafasi ya kumtetea mteja wao.
Hivi sasa Moise Katumbi hayuko nchini Kongo, bali yuko barani Ulaya kwa ajili ya matibabu kwa zaidi ya wiki tatu sasa.
Kabla ya hapo, mwendesha mashtaka mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliruhusu Moise Katumbi aende Afrika Kusini kwa matibabu, hata hivyo baada ya kufika Afrika Kusini, mgombea huyo urais wa muungano wa wapinzani wa Kongo aliamua kuelekea barani Ulaya kwa matibabu zaidi.