Kaduma: Ni vyema Sheni angekubali kushindwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i979-kaduma_ni_vyema_sheni_angekubali_kushindwa
Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Ibrahim Kaduma ameungana na wanasiasa na shakhsia wengine mashuhuri nchini humo ambao wanapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa maelezo kuwa maridhiano baina ya pande zinazopingana yana nafasi nzuri ya kutatua mgogoro uliopo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2016 11:54 UTC
  • Kaduma: Ni vyema Sheni angekubali kushindwa

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Ibrahim Kaduma ameungana na wanasiasa na shakhsia wengine mashuhuri nchini humo ambao wanapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa maelezo kuwa maridhiano baina ya pande zinazopingana yana nafasi nzuri ya kutatua mgogoro uliopo.

Kaduma, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ya hayati Mwalimu Julius Nyerere ameviambia vyombo vya habari kama ninavyomnukuu: “Katika suala la Zanzibar nadhani CCM tungekubali kushindwa. Mimi ni mwanaCCM lakini nasema tungekubali kushindwa. Ningekuwa (Dk Ali Mohamed) Shein ningelinda heshima yangu maana hii ni hatari,” amesema mwanasiasa huyo mkongwe.

Mzee Kaduma amesema kwa kuwa suala la Zanzibar ni baina ya vyama vya CCM na CUF, na mtu pekee wa kutafuta ukweli ni mwenyekiti wa CCM.

“Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuweka mambo ya Zanzibar sawa maana yeye ndiye mwenyekiti wa CCM na suala lenyewe linakihusu CCM na CUF, ingawa kwa mbali sana Magufuli naye anaweza kufanya lolote kuondoa tatizo lililopo,” amesisitiza mwanachama huyo mkongwe wa CCM.

Amesema anaamini CCM ingetenda haki kama ingepokea matokeo kama yalivyokuwa ambayo hata waangalizi wa ndani na nje wamesema hayakuwa na dosari. “Ni vyema Rais Shein angekubali kushindwa. Chama pia kingefanya hivyo. Huko ndiko kujisahihisha. Kufanya hivyo Rais Shein angeondoka na heshima yake.” amesema Mzee Ibrahim Kaduma.

Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo ZEC Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.

Hatua hiyo ilichukuliwa katika hali ambayo matokeo yote ya uchaguzi wa majimbo 54 ya Baraza la Wawakilishi yalikuwa yameshatangazwa pamoja na karibu theluthi mbili ya kura za Urais.

Mwenyekiti huyo wa ZEC ametangaza tarehe 20 ya mwezi ujao wa Machi kuwa siku ya kufanyika uchaguzi wa marudio ambao umesusiwa na vyama tisa kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, kikiwemo chama cha CUF ambacho kinadai mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif ndiye mshindi halali wa kiti hicho…/