Jun 04, 2023 11:32 UTC
  • Museveni: Wanajeshi 54 wa Uganda wameuawa na al-Shabaab Somalia

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema makumi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (UPDF) waliuawa katika shambulio la wanamgambo wa al-Shabaab nchini Somalia wiki iliyopita.

Museveni amesema, katika shambulio hilo la Ijumaa ya wiki iliyopita dhidi ya askari wa UPDF wanaohudumu chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), askari 54 wa Uganda waliuawa. 

Hata hivyo, genge hilo la kigaidi na ukufurishaji lilidai kuwa liliua wanajeshi zaidi ya 137 wa Uganda kwenye hujuma hiyo.

Inaarifiwa kuwa, magaidi wa al-Shabaab waliokuwa wamejifunga mabomu walijiripua na kuingia kwa nguvu kwenye kambi hiyo ya kijeshi ya askari wa Uganda katika eneo la Bulo-Mareer. 

Rais Museveni amesisitiza kuwa, Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo UPDF litatoa jibu kali kufuatia shambulizi la wanamgambo wa al-Shabaab. Kadhalika amelipongeza jeshi hilo kwa kujikusanya na kuikomboa kambi hiyo iliyokuwa imetekwa na magaidi wa al-Shabaab.

Rais Museveni wa Uganda

Awali Rais wa Uganda alikosoa mchakato mzima wa kuwateua wanajeshi wa Uganda wanaotumwa nchini Somalia na kusisitiza kuwa, baadhi ya wanajeshi hawakuwajibika ipasavyo, na kwamba baadhi yao waliingiwa na wahaka ndiposa wakashambuliwa vibaya na al-Shabaab.

Maelfu ya walinda usalama wa Umoja wa Afrika wameuawa huku mamia wakijeruhiwa nchini Somalia tangu walipoingia nchini humo mnamo mwaka wa 2007. Tangu mwaka huo wa 2007, wanajeshi wa AU walioorodheshwa kuuawa ni takriban 4,000.  

Tags