Uganda yatangaza tarehe ya kuondoa askari wake Somalia
Uganda imetangaza kuwa itaondoa askari wake walioko nchini Somalia chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM kufikia mwishoni mwa mwaka ujao 2017.
Jenerali Katumba Wamala, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda UPDF amesema serikali ya Kampala imechukua uamuzi huo kutokana na ukosefu wa ushirikiano na muamala mzuri kati ya askari wake, jeshi la Somalia na washirika wa kimataifa. Amesema yumkini Uganda ikaondoa vikosi vyake nchini Somalia kabla ya Disemba mwaka ujao iwapo nchi yeyote ya Kiafrika itajitolea kutuma wanajeshi wake kujaza nafsi ya UPDF.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, kuna zaidi ya wanajeshi elfu sita 6,000 wa Uganda ambao wanatekeleza jukumu la kulinda amani nchini Somalia chini ya AMISOM katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Haya yanajiri siku chache baada ya Kenya kutishia kuwaondoa askari wake zaidi ya 4,000 ambao wako nchini Somalia chini ya kikosi cha AMISOM kutokana na kile Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo ilikitaja kuwa, vizingiti vya nchi zinazofadhili shughuli za kikosi hicho cha kulinda amani Somalia. Mapema mwezi Machi mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulisema utapunguza asilimia 20 ya misaada yake kwa kikosi hicho.
Askari elfu 22 wa Afrika walitumwa nchini Somalia miaka 9 iliyopita kwa ajili ya kurejesha amani na kukabiliana na kundi la kigaidi la al Shabab.
Mfuko wa kusaidia amani barani Afrika unaosimamiwa wa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka 9 iliyopita umechangia zaidi ya yuro bilioni moja kwa ajili ya bajeti ya AMISOM.